Scolastica Msewa, Moshi – Kilimanjaro.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo, Mifugo na Uvuvi ikiongozwa na Mwenyekiti wa kamati hiyo Mbunge wa Njombe Mjini, Deo Mwanyika wamepongeza jitihada zinazofanywa na Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), katika kuhakikisha kiwanda cha KMTC kinaboreshwa na kuendelea na uzalishaji wa vipuli pamoja na mashine mbalimbali, kama ilivyokusudiwa wakati wa uanzishaji wake.

Pongezi hizo zimetolewa mara baada ya Kamati hiyo ya kudumu ya Bunge kutembelea kiwanda hapo na kukagua shughuli mbalimbali zinazofanyika katika kiwanda hicho kilichopo wilayani Hai mkoani Kilimanjaro.

Mwanyika amesema, KMTC ni kiwanda kikubwa cha kuzalisha viwanda vingine na kina mchango mkubwa kwenye uchumi huku akibainisha kuwa malighafi kubwa ya kiwanda hicho ni chuma kinachotumika kutengeneza vipuri na mashine na kama Taifa tukitaka tufikie malengo lazima tuanze Uchimbaji wa chuma cha Liganga.

“Nimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuona umuhimu wa kiwanda hiki kwenye matumizi ya chuma, hivyo kuamua kutoa fedha za fidia kule Liganga ili chuma kile kitumike kiwandani hapa,” amesema Mwanyika.

Kwa upande wake Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Ashatu Kijaji amesema wao kama Wizara yenye dhamana ya kusimamia maendeleo ya viwanda hapa nchini wanafurahi kuona kazi ya kuyeyusha chuma imeanza kiwandani hapo hivyo kurejesha ajira kwa Watanzania ambao walikosa ajira kwa muda mrefu.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), Dkt. Nicolaus Shombe alisema bidhaa zinazozalishwa na KMTC zinagusa sekta mbalimbali kama kilimo, viwanda, uchukuzi, usafirishaji, madini, misitu na ujenzi hivyo kuwa ni kiwanda chenye manufaa katika sekta hizo.

Dkt. Shombe amebainisha kuwa, Serikali imeendelea kufanya juhudi mbalimbali, ili kuhakikisha kiwanda hiki kinaboreshwa na hatimaye kiweze kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya viwanda nchini na kuinua maisha ya wananchi na kutoa ajira ambapo mpaka hivi sasa ujenzi wa tanuru la kuyeyusha chuma pamoja na mtambo wa kutia utandu kwenye chuma umeshakamilika.

Dkt. Biteko: Uwekezaji sekta ya Elimu lazima umguse Mwalimu
ASDP II kuleta mapinduzi sekta ya Kilimo