Kocha Mkuu wa Simba SC, Abdelhak Benchikha amerejea nchini kutoka kwenye mafunzo ya siku tano ya kuongeza ujuzi alonao, huku akitoa kauli inayoweza kuwapa mzuka Mashabiki na Wanachama wa klabu hiyo, kwa kusema licha ya kupangwa na Mabingwa Watetezi wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, Al Ahly ya Misri, hana presha nao kwa vile wanaijua na kwamba watakula nayo sahani moja.
Simba SC imepangwa kukutana na Al Ahly katika mechi ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa baada ya Droo iliyofanyika juzi Jumanne (Machi 12) jijini Cairo, iliyoshuhudiwa pia Young Africans ikipewa Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, huku TP Mazembe ikikabidhiwa kwa Petro Atletico ya Angola na Esperance ya Tunisia ikipangwa kuvaana na Asec Mimosas ya Ivory Coast.
Tangu Droo hiyo ilipofanyika, kumekuwa na mijadala mitandaoni kutoka kwa wadau wa soka wakiamini Simba SC na Young Africans zimekutana na vigingi katika mbio za kutaka kuandika historia ya kucheza Nusu Fainali ya michuano hiyo, lakini Benchikha amesema, hana presha na wapinzani aliopewa katika hatua hiyo ya Robo Fainali na kuwatuliza wanasimba.
Hii itakuwa ni mara ya nne kwa Simba SC na Al Ahly kukutana katika mechi nane za kimataifa, baada ya awali kukutana mara mbili kwenye makundi ya Ligi ya Mabingwa 2018-2019 na 2020-2021, kisha msimu huu zimekutana katika mechi za Robo Fainali ya michuano mipya ya African Football League ‘AFL’.
Katika mechi hizo sita za awali, Simba SC imeshinda mechi mbili nyumbani na kupoteza pia mbili ugenini, wakati katika AFL hakuna aliyeibuka mbabe baada ya kutoka sare ya 2-2 jijini Dar es salaam na 1-1 jijini Cairo na Al Ahly kuvuka kwa kanuni ya mabao mengi ya ugenini.
Simba SC itakuwa mwenyeji wa Al Ahly katika mechi ya mkondo wa kwanza ya Robo Fainali itakayopigwa kati ya Machi 29 na 30 kisha kurudiana na wababe hao wa Afrika kati ya Aprili 5 na 6 kuamua timu ya kwenda Nusu Fainali, lakini kocha Benchikha amesema anawafahamu vyema wapinzani hao na wao pia wanamfahamu vizuri kwani ndiye aliyewatoa katika michuano ya Super Cup ya Afrika miezi mitano iliyopita.
Benchikha amesema ameiona Droo ya kukutana na Al Ahly na wala hana presha na hizo mechi mbili, kwani anaamini atakaa na viongozi wake na wachezaji ili kujipanga vizuri.
Amesema anawajua Al Ahly anawaheshimu, ni timu yenye rekodi kubwa na matokeo yale alipokutana nao mwaka jana ana mpango wa kuyarudisha tena hata kwenye mashindano haya kwani uwezo huo anao.
“Ahly wanajua kuwa wanakwenda kukutana na mpinzani mgumu kwa kiasi gani na Simba SC itakwenda kupigania nafasi ya kwenda Nusu Fainali na sio kuhofia hadhi yao. Tunatakiwa kujipanga kwenda kuthibitisha kwa nini tupo kwenye klabu kumi bora Afrika kwa kushindana na klabu namba moja na bila hofu kila kitu kinawezekana,” amesema Benchikha.
Rekodi zinaonyesha kuwa, Simba SC imekuwa ikifanya vizuri mechi za nyumbani jambo linalompa jeuri kocha Benchikha aliyeitungua Al Ahly katika mechi ya CAF Super CAF iliyopigwa msimu huu akiwa na USM Alger kabla ya kujiuzulu na kuibukia Simba SC na kuivusha timu hiyo katika hatu ya Robo Fainali ya tano katika misimu sita tofauti ya CAF iliyoshiriki.