Serikali Nchini, inaendelea kutoa ushirikiano kwa wadau mbalimbali katika masuala ya uratibu wa maafa ili kuendelea kujiandaa kisha kukabili kwa wakati na kupunguza madhara yanayoweza kutokea pindi maafa yanapotokea.
Mkurugenzi Msaidizi, Kituo cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura, Idara ya Menejimenti ya Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Jane Kikunya wakati akifungua Warsha ya siku moja iliyowakutanisha wadau kutoka Serikalini, Makampuni ya simu, Taasisi zinazotoa Misaada ya kibinadamu.
Misaada hiyo, hutolewa kwa lengo la kujadili fursa na kutoa maoni kuhusu njia sahihi ya ujumuishaji wa teknolojia ya simu katika mifumo ya kutoa tahadhari ya Awali (Early Warning System – EWS) iliyofanyika jijini Dodoma.
Amesema, kampuni na taasisi mbalimbali zinatakiwa kuendelea kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali katika mzingo wa menejimenti ya maafa, ikiwemo wa kuzuia, kujiandaa, kukabili na kurejesha hali pindi maafa yanatokea.
“Tumieni warsha hii kwa matokeo chanya yaliyokusudiwa kwa kuongeza ujuzi na kushirikishana uzoefu katika masuala yanayohusu fursa mbalimbali kuhusu njia sahihi za kutumia teknolojia ya simu katika mifumo na kutoa taarifa za tahadhari za awali ili kuendelea kuwa na utayari katika kukabili maafa,” alisema Jane.
Aliongeza kuwa, Tanzania imekuwa ikikumbwa na maafa ya asili na yale yasiyo ya asili ikiwemo ya mafuriko, matetemeko ya ardhi, moto, maporomoko ya tope na mawe, ukame, upepo mkali, magonjwa ya milipuko kwa binadamu na wanyama, hivyo kupitia warsha hiyo wazingatie umuhimu wa taarifa za tahadhari za awali, ili kuendelea kujiandaa kisha kukabili kwa wakati na kupunguza madhara wakati wa maafa.
“Na taarifa za awali zinaipa jamii uelewa wa kuchukua hatua za awali kabla ya madhara ya maafa kuwa makubwa hivyo upo umuhimu wa kuendelea kuzijengea uwezo jamii juu ya matumizi sahihi ya taarifa hizo,” alisema.
Warsha hiyo imehudhuriwa na wataalam kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Wizara ya Mifugo, Wizara ya Maji, Wizara ya Afya, Wizara ya Kilimo pamoja na Taasisi ikiwemo TCRA, TMA, REDCROSS, makampuni ya simu pamoja na Airtel, Vodacom, Tigo/Zanztel.