Beki wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans, Dickson Job amefunguka jukumu lake kubwa akiwa anaingia uwanjani ni kupambana kukaba kwa asilimia zaidi ya 100 kuhakikisha haruhusu bao.
Akizungumza jijini Dar es salaam, Job amesema jukumu lake kubwa ni kuhakikisha haruhusu bao kwa njia yoyote kuweza kulinda timu yake.
“Asilimia 60 au 70 za ushindi katika timu ni kutoruhusu bao, kabla ya sisi kufunga hatutakiwi kuruhusu goli ili tuwe na nafasi kubwa ya kupata goli.
“Kama ikitokea tutaruhusu goli tayari tunakuwa tumeruhusu mchezo uwe katika hali ngumu, hivyo tunapoingia uwanjani kila mmoja anatambua majukumu yake,” amesema Job
Amesema presha inakuwepo kama walinzi kutokana na kuwa ni nafasi waliyochagua na ndiyo kazi yao, hivyo wanatakiwa kupambana kuhakikisha timu inapata matokeo.
Job amesema inapotokea wanafanya makosa ya kizembe, Mlinda Lango wao Djigui Diarra, huwa ni mkali sana na wakati mwingine huwafokea kwa makosa yao ya kizembe.
“Ikitokea kuna makosa ya kizembe Diarra huwa anafoka sana, lakini mimi namuelewa hii ni kazi, hivyo tunapaswa kupambana kupunguza makosa,” amesema