Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’ imetegua kitendawili cha tarehe za kuchezwa kwa Michezo ya Robo fainali, Ligi ya Mabingwa Barani humo msimu huu,m kwa timu za Simba SC na Young Africans.
Awali CAF ilitangaza Machi 29 au 30 kuwa tarehe maalum za michezo ya mkondo wa kwanza ya Robo Fainali, huku April 05 na 06 zikitajwa kama tarehe za michezo ya mkondo wa pili, bila kuweka michezo husika katika tarehe hizo, hali iliyoweka mkanganyiko kwa timu hizo zinazotumia uwanja wa Benjamin Mkapa.
Leo Ijumaa (Machi 15) CAF wameainisha ratiba maalum ya hatua ya Robo Fainali kwa kutaja michezo husika kwa tarehe husika, huku Simba SC ikipoangiwa kucheza Ijumaa (Machi 29) dhidi ya Al Ahly ya Misri, katika uwanja wa Benjamim Mkapa jijini Dar es salaam, majira ya saa tatu usiku.
Young Africans itaikaribisha Mamelodi Sundowns Jumamosi (Machi 30) katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, majira ya saa tatu usiku.
Hata hivyo bado michezo ya mkondo wa pili kwa Simba SC na Young Africans, bado imebaki kama ilivyokuwa imepangwa, ambapo wenyeji Al Ahly (Misri) na Mamelodi Sundowns (Afrika Kusini) wataamua ichezwe kati ya April 05 au 06.