Mshambuliaji wa timu ya Tanzania Prisons ya jijini Mbeya, Samson Mbangula amewataja walinzi Dickson Job, Erasto Nyoni na Juma Said ‘Nyoso’ kuwa ni miongoni mwa mabeki ambao wanampa shida anapokuwa
Mbangula ambaye amepachika mabao manane katika mechi za msimu huu za Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara (TPL) akiwa na maafande wa Prisons kuwa akikutana na walinzi hao anakuwa katika wakati mgumu.
Amefafanua kuwa wapo mabeki wengi katika ligi hiyo, wanamsumbua uwanjani wakati akitekeleza majukumu yake.
“Kuna baadhi ya walinzi katika msimu huu wa TPL, ambao wananipa shida mno uwanjani. lla Job, Nyoni na Nyoso, hawa jamaa ni balaa zaidi kwangu,” amesema mshambuliaji huyo.
Amesema Job licha ya udhaifu wake, lakini ana nguvu na anacheza kwa ufundi mkubwa uwanjani, wakati Nyoni, yeye siyo beki anayependa sana kugongana uwanjani anachotaka ni kunyanganya mpira.
Mchezaji huyo amesema kuwa beki Nyoso, ni miongoni mwa walinzi wanaotumia nguvu uwanjani, hivyo ukitaka kumpita mlinzi huyo (Nyoso) lazima mshambuliaji uwe timam kimwili.
Akizungumzia uwezekano wa kuzichezea klabu za jijini Dar es salaam Young Africans, Simba SC na Azam FC amesema anaamini hakuna kitu kinachoshidikana chini ya jua.
Amesema licha ya kuwa mwajiriwa wa Jeshi la Magereza, lakini hakutamzuia kufanya mabadiliko endapo kama viongozi wa klabu hizo watafuata mchakato unaostahili wa usajilil.
“Mpaka sasa ninavyoichezea Tanzania Prisons ya Mbeya katika ligi, mimi ni mwajiriwa wa Jeshi la Magereza Tanzania. Lakini hilo katu siyo kikwazo kusajiliwa klabu nyingine, endapo kama zitafuata utaratibu sahihi wa usajili,” amesema