Mshambuliaji Mohamed Salah amekuwa mchezaji wa kwanza wa Liverpool kufunga mabao 20+ kwa misimu saba mfululizo akiandika rekodi tamu kabisa katika maisha yake ya soka.
Raia huyo wa Misri, alikuwa kwenye kiwango bora sana wakati Liverpool iliposhusha kipigo kizito kwa Sparta Prague kwenye mechi ya marudiano ya michuano ya Europa League, juzi Alhamis (Machi 14).
Baada ya Darwin Nunez na Bobby Clarke kufunga kwenye dakika nane za kwanza, Mo Salah naye alionyesha maajabu yake.
Jambo hilo limemfanya Mo Salah mwenye umri wa miaka 31, sasa awe amefunga mabao 20 na kuasisti 10 katika michuano yote msimu huu.
Huu ni msimu wa saba kwa Mo Salah kufunga walau mabao 20 na kuendelea kwenye kikosi hicho cha Liverpool na rekodi zinaonyesha hakuna mchezaji wa timu hiyo aliyewahi kufanya hivyo.
Huko nyuma Ian Rush, ndiye aliyekuwa akishikilia rekodi ya kufunga mabao 20+ kwenye misimu sita mfululizo kati ya msimu wa 1981-82 na 1986-87.
Kiwango hicho cha Mo Salah kimekuja wakati mwafaka ambapo kocha Jurgen Klopp anamhitaji kweli kweli kwenye mchezo wa Kombe la FA dhidi ya Manchester United kesho Jumapili (Machi 17).
Baada ya bao la Salah, Liverpool iliendelea kuifanyia kitu kibaya Sparta Prague.
Fowadi wa Kidachi Cody Gakpo alifunga mara mbili kwenye ushindi huo wa 6-1 na kufanya Liverpool kutinga Robo Fainali kwa jumla ya mabao 11.
Bao jingine la Liverpool kwenve mchezo huo lilifungwa na Dominik Szoboszlai.
Tayari Liverpool imeshamtambua mpinzani wake katika hatua ya Robo Fainali ya Europa League, baada ya kupangwa kwa Droo ya Michuano hiyo jana Ijumaa (Machi 15), mjini Nyon nchini Uswiz.
Liverpool imepangwa kucheza na Atalanta ya nchini Italia, mchezo wa mkondo wa kwanza ukitarajiwa kuchezwa April 11.
Michezo mingine ya Robo Fainali ya Europa League.
AC Milan – Roma
Bayer Leverkusen – West Ham United
Benfica – Marseille