Mchezo wa Robo Fainali, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Al Ahly ya Misri umemuibua Kiungo kutoka nchini Zambia na Klabu ya Simba SC Clatous Chama, huku akisema hautakuwa mchezo rahisi.

Jumanne (Machi 12) Simba SC ilipangwa kukutana na Al Ahly baada ya kuchezeshwa kwa Droo ya Robo Fainali, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, mjini Cairo-Misri.

Chama amesema Simba SC inapaswa kuwaheshimu Al Ahly kutokana na ubora walio nao, lakini hawana budi kujipanga kuhakikisha wanaibuka na ushindi kwenye mchezo huo, utakaopigwa jijini Dar es salaam Machi 29 kabla ya kupigwa tena mjini Cairo, Misri April 05 au 06.

Amesema Simba SC imeshakutana mara kadhaa na Al Ahly na anaamini ni muda mzuri kwa timu yake kuandika historia ya kuwang’oa Mabingwa hao wa kihistoria kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.

“Mchezo dhidi ya Al Ahly utakuwa mgumu, kwanza tunatakiwa kuwaheshimu wapinzani wetu kwa sababu ni timu kubwa, tutawaheshimu lakini hatuwaogopi.”

“Kikubwa tumeshacheza nao mara kadhaa, nahisi sasa ni muda na sisi kuandika historia, tunatakiwa tufahamu kuwa ile timu tunayocheza nayo huwa inafika fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, kwa hiyo tunatakiwa kuwa makini na tumuombe mungu atusaidie, atulinde na hiyo siku ya mchezo wote tuamke vizuri, ili tucheze vizuri.” amesema Chama

Miezi mitano iliyopita, Simba SC na Al Ahly walikutana katika michuano mipya ya African Football League na Wekundu wa Msimbazi iliondolewa kikanuni.

Katika mechi ya kwanza iliyochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Oktoba 21, mwaka jana, timu hizo zilitoka sare mabao 2-2 na waliporudiana Oktoba 24, zikatoka tena sare ya bao 1-1, na Simba SC kutolewa kwa kanuni ya mabao ya ugenini.

Pia zilikuwa pamoja kwenye hatua za makundi msimu wa 2018/19 zikiwa Kundi D na zote zikasonga mbele hatua ya Robo Fainali, AI Ahly ikiongoza kundi, Simba SC ikifungwa mabao 5-0 ugenini na kushinda bao 1-0 nyumbani.

Mara nyingine tena ilikuwa hatua ya makundi msimu wa 2020/21, kila timu ikishinda bao 1-0 nyumbani, zote mbili zikisonga mbele, Simba SC ikiongoza kundi hilo.

Man City yasitisha hadithi ya De Bruyne
Kevin De Bruyne atemwa Ubelgiji