Scolastica Msewa, Kibaha – Pwani.
Makarani waongozaji wa Uchaguzi wamepata Mafunzo pamoja na kuapa kiapo cha kutunza Siri chini ya Kanuni ya 16(1) (a) na 50 (4) ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais na Wabunge, 2020 na Kanuni ya 14 (1)(a),(2) na 43(4) ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa (Uchaguzi wa Madiwani), 2020 Mbele ya Msimamizi wa Uchaguzi Salum Papen.
Mafunzo hayo yametolewa na Maria Israel, Benjamin Mputtu wakisaidiana na Afisa Uchaguzi wa Halmashauri ya Mji Kibaha, Optuna Kasanda ambao wamewasisitiza kwenda kufanyakazi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na taratibu za Uchaguzi.
Akifungua Mafunzo hayo, Msimamizi wa Uchaguzi, Mwanasheria wa Mahakama Kuu Salum Papen ametoa rai kwa Makarani waongozaji kujiamini na kufanya kazi kwa kuzingatia Katiba ya Nchi, Sheria za Uchaguzi na Kanuni zake, Maadili ya Uchaguzi na Maelekezo mbambali yanayotolewa na Tume.
Katika hatua nyingine Makarani wametia tamko la kujitoa uanachama au kutokuwa na Chama cha Siasa chini ya Kanuni ya 16 (1)(b) na ( 3 ) ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais na Wabunge,2020 na Kanuni 14(1) (b) na (3) ya Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, (Uchaguzi wa Madiwani), 2020.
Naye, Andrea Isamaki Ofisa kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ameshiriki kushuhudia Mafunzo,kiapo cha kutunza Siri na tamko la kujitoa uanachama kwa Makarani waongozaji
Nadya Issa na Benson Shawa, Makarani waongozaji wamesema wanakwenda kufanya kazi kwa weledi mkubwa kwa kuzingatia Sheria,Kanuni na taratibu za Uchaguzi.
Uchaguzi mdogo Kata ya Msangani unafanyika kutokana na kifo cha Leonard Mlowe kilichotokea Desemba 23, 2023 ambapo jumla ya vyama nane vya Siasa vinatarajia kushiriki siku ya Jumatano Machi 20, 2024.