Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI imetembelea Gereza la Wilaya ya Chato kwa lengo la kujionea namna mwitikio wa UKIMWI unavyotekelezwa katika gereza hilo ambapo wamekutana na mahabusu, Wafungwa, Askari, Maafisa pamoja watumishi wa umma.
Akizungumza katika ziara hiyo ya mwishoni mwa wiki Mkoani Geita, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, Stanslaus Nyongo alisema Kamati imeridhishwa na jinsi Magereza inavyopanga na kutekeleza mikakati ya Mwitikio wa UKIMWI katika gereza hilo.
Alisema utekelezaji wa afua za Mwitikio wa UKIMWI katika gereza la Chato zinaridhisha ambapo alimpongeza Mkuu wa Jeshi la Magereza kutokana na kuhakikisha Wafungwa na Mahabusu wanakuwa salama kiafya.
“Nitumie nafasi hii kumshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwani kila kinachofanyika ni kutokana na mwongozo na maelekezo yake. Pia niwasisitize kuchukua tahadhari ya maambukizi ya VVU ikiwa ni pamoja na kupima afya kwa wale ambao hawajapima ili mjue afya zenu, pamoja na kuanzishiwa dawa kwa wale ambao watagundulika kuwa na maambukizi ya VVU,” alisema Nyongo.
Aidha, aliiomba Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS), kuangalia namna ambavyo itaandaa mkakati maalum wa kutekeleza afua za UKIMWI katika magereza yote nchini ikiwa ni pamoja na kuwajengea uwezo maafisa magereza katika utoaji elimu ya VVU katika maeneo yao.
Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Ummy Nderiananga alisema Ofisi ya Waziri Mkuu inapokea maagizo yote yanayotolewa na Kamati hiyo, kwa ajili ya Utekelezaji.