Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, imeielekeza Menejimenti ya Hifadhi ya Taifa Saadani kuandaa mpango mahususi wa kuainisha maeneo ya uwekezaji ili kuvutia wawekezaji.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Timotheo Mnzava ameyasema hayo wakati wa ziara ya Kamati hiyo ya kukagua miradi katika Hifadhi ya Taifa Saadani iliyopo katikati ya pembe tatu za miji ya Tanga,Bagamoyo na Mji Mkongwe wa Zanzibar.
Amesema, menejimenti hiyo inatakiwa kufanya ukarabati wa miundombinu hasa ya barabara, ujenzi wa gati na uwanja wa ndege katika eneo la hifadhi hiyo.
Wakichangia kwa nyakati tofauti, baadhi ya wajumbe wa Kamati hiyo wameelekeza TANAPA kutangaza uwekezaji wa maeneo ya fukwe pamoja na kuongeza vivutio vya utalii katika hifadhi ya Saadani.
Kwa upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki amesema Serikali inaona umuhimu wa kuwa na mpango wa maeneo ya Uwekezaji hivyo, hifadhi zimeshaelekezwa kuandaa na mpango mahususi wa muda mrefu wa maeneo ya uwekezaji.
Kuhusu pendekezo la kuboresha miundombinu, Waziri Kairuki amesema Wizara ya Maliasili na Utalii inaangalia namna ya kuweka fedha zaidi katika kuboresha uwanja wa ndege, barabara ndani ya hifadhi na kufuatilia ujenzi wa gati.
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi amesema kuwa Serikali inaandaa mkakati wa kuendeleza zao la utalii wa fukwe ambao utaainisha maeneo yote ya fukwe kwa ajili ya uwekezaji.