Huku wengi wakiipa nafasi zaidi Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini kwenye mechi ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Young Africans Jumamosi (Machi 30), Kocha Mkuu wa Young Africans, Miguel Gamondi, ameichambua timu hiyo na kusema hakuna lisilowezekana kwa kuwa watakuwa 11 kwa 11 uwanjani na si vinginevyo.
Young Africans itaikaribisha Mamelodi katika Uwanja wa Benjamin Mkapa na baada ya hapo timu hizo zitarudiana Aprili 5, mwaka huu, nchini Afrika Kusini na mshindi wa jumla atatinga Nusu Fainali ya michuano hiyo mikubwa zaidi kwa ngazi ya klabu barani Afrika.
Akiwachambua wapinzani wao hao, Gamondi amesema ubora wa kikosi na bajeti ya usajili wa Mamelodi Sundowns ni tofauti na Young Africans, lakini hilo haliwapi woga, badala yake wanahitaji kupambana na kuweka juhudi zaidi katika mchezo huo wa nyumbani.
Gamondi amesema anafahamu misingi ya Mamelodi kwa sababu ni timu yake ya zamani na wamekuwa bora sana kwa msimu huu 2023/24, na kwamba waliongeza mchezaji kutoka Argentina kwa usajili ghali tofauti na wao ambao dirisha dogo waliwaleta Joseph Guede na Augustine Okrah wakiwa wachezaji huru.
Amesema kuna tofauti kubwa ya Mamelodi Sundowns na Young Africans, ila ni wakati maalum kwao kuonyesha ubora na ili kufikia ukubwa huo wa kuwa miongoni mwa timu tano bora Afrika, lazima wapambane kushinda mechi hiyo.
“Tunahitaji kupigana, kuweka juhudi zaidi kuliko Sundowns, kama nilivyosema awali tulipocheza na Al Ahly, suala la uzoefu lilituathiri kidogo, pia bajeti ukilinganisha na yetu ni tofauti, lazima watu waelewe, lakini haijalishi kwani mpira ni dakika 90 na wote tunacheza 11 dhidi ya l1,” amesema kocha huyo
Amesema wanatakiwa kuweka juhudi kubwa kuhakikisha wanapambana na timu bora yenye wachezaji wenye uzoefu mkubwa.
Ameongeza kuwa miaka ya hivi majuzi, Mamelodi Sundowns imekuwa ikipata wapinzani wengi kutoka Afrika Kaskazini katika michuano ya Ligi ya Mabingwa, mara ya mwisho kuwa na upinzani Kusini mwa Jangwa la Sahara ilikuwa msimu wa 2021/22 walipotupwa nje na wababe wa Angola, Petro Atletico, hivyo ni zamu ya Young Africans kwa kuhakikisha wanashinda mechi ya kwanza ya nyumbani.