Machi 20, 1978, Mahakama ya Rufaa ya Tanzania ilimpunguzia kifungo cha jela Juma Thomas Zangira, Mtanzania wa kwanza kutiwa hatiani kwa kosa la kufanya ujasusi ndani ya Tanzania.
Majaji Francis Nyalali, Robert Kisanga na Kahwa Lugakingira walimkuta na hatia Zangira lakini walieleza kuwa kifungo cha miaka 20 jela ni adhabu kubwa kwa mshtakiwa kama yeye kutokana na jinsi alivyotoa ushirikiano katika kesi hiyo.
Aidha, walidai pia kutokuwepo kwa ushahidi wa kuthibitisha kwa uhakika athari ambazo Tanzania ingezipata kutokana na kosa alilolifanya Mshitakiwa huyo na ikawa ni kesi ya aina yake iliyowaacha Wananchi wakiwa hawaamini masikio yao, kwani ilikuwa ni ya kwanza ya ujasusi nchini.
Mtanzania huyo, Juma Zangira alidaiwa kutuma taarifa za kijasusi kwa mzungu mmoja na jajusi wa Kimataifa aitwaye John Wilson ambazo zingeharibu jitihada za TANU na vyama vya ukombozi vya SWAPO, FRELIMO, PAC, ANC na ZANU mashtaka yaliyodaiwa kuwa ni kinyume na Kifungu cha 9(1)(a) na 9(2)(1) vya Sheria ya Usalama wa Taifa, 1970.
Mshtakiwa Zanzira, aliyekuwa akitetewa na wakili Thomas Mkude wa lililokuwa Shirika la Sheria Nchini – TLC, alikana mashtaka yote ambayo ilidaiwa kuyatenda kati ya mwaka 1971 na Julai 1977.
Awali, akijitetea Zangira alisema alikuwa anamtumia Wilson habari za biashara zisizo na mashiko, huku wakili wa Zangira Mkude akiiomba Mahakama imuhurumie mteja wake kwani hilo ni kosa lake la kwanza na anategemewa na nduguze.
Akisoma hukumu hiyo, Jaji Nyalali alimtia hatiani Zangira kwa makosa matatu aliyoshtakiwa nayo akisema alikuwa ni Jasusi aliyekuwa akitumiwa na mataifa fulani, ili kuangamiza usalama wa Taifa.
Juma Thomas Zangira alikuwa ni Afisa Uhusiano wa Kilimanjaro hotel, Afisa Usalama wa Taifa na mmoja wa Watanzania wachache waliokuwa wamepata mafunzo ya aina yake ya ukomandoo toka nchi mbalimbali duniani.
Alikuwa ni Komandoo shupavu na mwenye ujuzi mkubwa wa mapambano katika ukanda wa Afrika. Mkono wake wa kushoto ulikuwa na nguvu za kipekee na alikuwa ni mbobevu kwenye masuala ya intelijensia aliyetunukiwa nishani nyingi kwa umahiri wake. Hivyo, alikuwa ni tegemeo kubwa kwa Taifa.