Shirika la afya duniani – WHO, limesema hatua za haraka zinahitajika, ili kukabiliana na ongezeko la ugonjwa wa Kipindupindu.
Tahadhari hiyo, imetolewa katika wakati ambapo Mataifa mengi yakikabiliwa na uhaba wa chanjo dhidi ya ugonjwa huo, huku Shirika la kimataifa la kuratibu usambazaji wa chanjo ICG, likidai kuelemewa na mahitaji.
ICG imesema, uzalishaji wa chanjo duniani kwa mwaka 2024 utakuwa kati ya dozi milioni 17 na milioni 50 japo idadi hiyo huenda ikawa ndogo ukilinganisha na mahitaji ya wagonjwa.
Idadi ya wagonjwa wa Kipindupindu waliorodeshwa na WHO mwaka 2022 iliongezeka mara mbili kutoka mwaka 2021 hadi wagonjwa 473,000 na kwa mwaka huu (2024), idadi imefikia wagonjwa 700,000.
Nchi zilizoathirika zaidi na ugonjwa huo ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo – DRC, Ethiopia, Haiti, Somalia, Sudan, Syria, Zambia na Zimbabwe.