Timu za Usimamizi wa Huduma ya Afya za Mikoa na Halmashauri, zimetakiwa kusimamia miradi ya afya inayotekelezwa katika maeneo yao na kuhakikisha vituo vyote vya kutolea huduma za afya ambavyo vimekamilika na havitoi huduma kwa wananchi vianze kufanyakazi mara moja.
Akizungumza na Timu ya Mkoa wa Geita, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI, anayeshughulikia afya, Dkt. Charles Mahera amesema Serikali imewekeza fedha katika kuboresha afyamsingi hivyo kila mtumishi anawajibu wa kuhakikisha miradi ya afya inakamilika kwa wakati na ubora.
Pia amewaonya viongozi hao kujiepusha na rushwa ambazo zinaleta taswira mbaya kwa jamii kuwa bila kutoa fedha huwezi kupata Huduma kwenye vituo vya kutolea huduma za afya vya Serikali.
Pia amewataka kuhakikisha wanafanya msawazo wa watumishi ndani ya halmashauri ili vituo ambavyo havina watumishi wa kutosha viweze kupata watumishi na kuanza kutoa huduma za msingi zinazohitajika kwa wananchi.