Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima ametoa wito kwa viongozi kuhakikisha udhibiti wa wimbi la watoto wanaokimbilia kuishi na kufanya kazi mitaani unaenda sambamba na kuimarisha Kamati za Ulinzi wa Watoto na Wanawake katika mamlaka za Serikali za mitaa.
Dkt. Gwajima ametoa wito huo kwa nyakati tofauti wakati wa ziara yake Wilaya za Kigamboni na Ilala Mkoani Dar Es Salaam kwa lengo la kufuatilia jinsi gani mkoa unadhibiti wimbi la watoto waishio na kufanya kazi mitaani.
Amebainisha kwamba, kwa mujibu wa Mpango kazi wa Taifa wa kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) kamati hizo zipo katika ngazi za kijiji, mitaa na kata ambapo, viongozi wa Serikali ngazi husika ndiyo wenyeviti na makatibu ni walimu au wataalamu wa kisekta.
Amesema, kundi kubwa la watoto hao lilipaswa kuwa shuleni lakini kutokana na changamoto mbalimbali zikiwemo kulegalega kwa kamati hizo zenye wajumbe wa kisekta, utoro wa watoto hao shuleni hukosa ufuatiliaji hadi ngazi ya kaya hivyo hukimbilia mitaani.
“Naombeni viongozi muhakikishe kamati za ulinzi wa wanawake na watoto zinapata idadi ya watoto waliotoroka shuleni sambamba na kubaini kaya wanazotoka ili kufanya uchambuzi wa mazingira ya kaya hizo na kuchukua hatua za maendeleo na ustawi wa jamii ili watoto hao wanaporejeshwa nyumbani wasitoroke tena,” alisema.
Aidha amesisitiza, Maafisa Maendeleo ya Jamii na Maafisa Ustawi wa Jamii wakishirikiana na Wadau wa maendeleo kusaidia kuchambua na kushauri juu ya ufumbuzi wa changamoto za kimaendeleo na kiustawi kwenye kila kaya wanakotokea watoto wanaoonekana kuwa na changamoto ili kudhibiti kabla watoto hao hawajakimbia shuleni na kwenye familia.

MAKALA: Kesho kuna matumaini zaidi kuliko jana
Malimwengu: 'Wachawi' 50 waamua kufa kwa pamoja