Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amesema ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato jijini Dodoma umefikia asilimia 54.1 kwa sehemu ya kwanza, inayohusisha ujenzi wa barabara ya kuruka na kutua ndege, maegesho ya Ndege, barabara za maungio na barabara za kuingia na kutoka kiwanjani ambapo unatarajiwa kukamilika Desemba, 2024.
Bashungwa ameyasema hayo wakati akiwasilisha Utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa mwaka wa fedha 2023/24 na Makadirio ya Mpango na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2024/25 kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu.
Amesema, ukarabati, upanuzi na uboreshaji wa Viwanja vya Ndege vingine umefikia hatua mbalimbali ambapo Iringa asilimia 90, Musoma asilimia 55, Tabora asilimia 38, Shinyanga asilimia 11, Sumbawanga asilimia 6 na Kiwanja cha Ndege cha Kigoma ambacho Mkandarasi bado yupo katika maandalizi ya kuanza ujenzi.
“Wakala wa Barabara (TANROADS) imefanikiwa kujenga barabara kwa kiwango cha lami zenye urefu wa kilometa 134.75 za barabara kuu, kilometa 23.11 za barabara za Mikoa na ukarabati kwa kiwango cha changarawe kilometa 253.67 katika kipindi cha utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2023/24,” alisema Bashungwa.
Aidha, ameitaja baadhi ya miradi iliyotekelezwa ikiwemo ujenzi wa Daraja la Kigongo-Busisi (km 3.2) na barabara unganishi (km 1.66) umefikia asilimia 85, ujenzi wa miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka Awamu ya Pili (km 20.3) umefikia asilimia 99.
Miradi mingine ni ujenzi wa barabara ya mzunguko wa nje Dodoma (km 112.3) sehemu ya kwanza umefikia asilimia 68.3 na sehemu ya pili ya utekelezaji umefikia asilimia 56.32, upanuzi wa madaraja ya kibamba, kiluvya na mpiji yamekamilika pamoja na upanuzi wa barabara ya Kimara-Kibaha (km 19.2) njia nane.