Kocha mpya wa Tabora United, Denis Goavec ameanza kazi rasmi kukinoa kikosi hicho lakini ameweka wazi mapungufu ya timu hiyo akianzia na safu ya ushambuliaji baada ya kufuatilia picha za televisheni za baadhi ya mechi.
Aidha, kocha huyo raia wa Ufaransa ameenda mbali na kusema tatizo lingine la timu yake ni namna ya kuunganisha timu na kutengeneza nafasi za kufunga.
Goavec amepewa jukumu la kukinoa kikosi cha Tabora United baada uongozi wa timu hiyo kuvunja mkataba na aliyekuwa kocha wao Mserbia, Goran Copunovic, ambaye hakuwa na wakati mzuri kwenye timu hiyo.
“Mimi ni mtu wa kutaka kupambana, nafanya kazi kwa malengo, ninachohitaji tuungane mimi, viongozi, wachezaji na mashabiki ili tuwe kitu kimoja kwa ajili ya kusaka ushindi.
“Nimengalia baadhi ya michezo na vipo vitu ambavyo nimevigundua tunahitaji kuvifanyia kazi, kwanza nimegundua safu ya ushambuliaji ina shida, timu inatengeneza nafasi chache na inafunga mabao machache, kwa hivyo lazima kwanza tuanze na yale mapungufu makubwa ambayo nimeyagundua,” amesema kocha huyo
Aidha, amesema atayafanyia kazi mapungufu yote na kujenga kikosi chenye uwiano sawa na anaamini kitafanya vizuri kwenye michezo iliyobaki mbele yao.
Aidha, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Klabu hiyo, Thabit Kandoro amesema wamefurahi sana kupata kocha huyo, akisema anaamini sasa kile ambacho wamekiwekeza kitaonekana uwanjani.
Amesema kwa muda mfupi tu wa kumtazama amegundua kuwa ni mtu ambaye anajua vitu vingi na mfuatiaji sana wa mambo na hiyo inatia moyo kuwa na kocha ambaye anaanza kazi na timu huku akiwa anajua mapungufu.
“Sisi tuna wachezaji 11 kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika, wametoka katika klabu kubwa kwa hiyo uwekezaji huu ni lazima uonekane uwanjani kitu ambacho tulikuwa hatukioni, baada ya kuongea na kocha huyu, kuna baadhi ya vitu ambavyo ametuambia, tumeona ni kweli anaweza akavifanya, nimeona siku ya kwanza tu amewaita mchezaji mmoja mmoja na nimefarijika kufahamu mipango yake,” amesema Kandoro.
Tabora United inashika nafasi ya 13 kwenye msimamo wa ligi ikiwa na alama 21, ikisalia na michezo tisa tu kuhitimisha msimu.