Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameitaka Wizara ya Uchukuzi kusimamia ipasavyo Shirika la Ndege Tanzania, ili kuhakikisha uwekezaji mkubwa uliofanywa unaleta matokeo chanya na kuwa kichocheo cha ukuaji wa sekta nyingine mtambuka na uchumi kwa ujumla wake.
Majaliwa ameyasema hayo alipomuwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye mapokezi ya ndege mpya aina ya Boeing 737-9 Max, jijini Dar es Salaam na kuongeza kuwa ongezeko la ndege na huduma za usafiri inasaidia kuongeza fursa za biashara kati ya Tanzania na mataifa mengine kuongeza upatikanaji wa fedha za kigeni na kuongeza idadi ya watalii wanaokuja nchini.
Amesema, ili kuendelea kuikuza sekta ya anga nchini, Wizara ya Uchukuzi iandae mpango wa kuongeza wataalamu wazalendo katika fani zinazohusu masuala ya ndege hususan katika eneo la matengenezo na urubani.
Majaliwa pia amewataka watumishi wa Shirika la Ndege Tanzania kuongeza uzalendo na kuwafichua wale wote wenye nia ya kulihujumu shirika hilo pamoja na kudhibiti upotevu wa mapato kupitia tiketi na mizigo huku akiwataka viongozi na watendaji wa Shirika hilo wahakikishe ndege zote zinaendeshwa kwa tija kwa kufanya tafiti za kutosha wa masoko kabla ya kupeleka ndege
Amesema, usafiri wa anga umekuwa chachu ya kuongeza mnyororo wa thamani wa mazao ya kilimo na biashara. “Uwepo wa usafiri wa ndege umeongeza tija kubwa kwa wakulima hususan wa mazao ya mbogamboga na matunda, wafugaji na wafanyabiashara wa Kitanzania.”