Serikali kupitia Wizara ya Kilimo, imewataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuzikamata Kampuni zote zinazodaiwa na Wakulima na kupandishwa kizimbani haraka iwezekanavyo.
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe ameyasema hayo katika Mkutano Mkuu wa Wadau wa zao la Tumbaku wa mwaka 2024 Jijini Dodoma na kudai kuwa kampuni na vyama vyote vya ushirika vinavyodaiwa zinatakiwa kulipa madeni haraka iwezekanavyo.
“Na kampuni zote ambazo zinadaiwa hazitakiwi kupewa leseni,nakumbuka tabora kuna baadhi ya kampuni zilikamatwa, kwaio naomba wakuu wa mikoa na Wilayani muwakamate kwa niaba ya Wakulima,” amesema.
“Na Wakuu wa Mikoa na Wilayani msije Mkatengeneze Uhusiano wa kibiashara mkamkandamiza Mkulima, tengenezeni Uhusiano wa kumnyanyua Mkulima,” amesema Bashe.
Hata hivyo amewataka Mameneja wa Vyama ndani ya wiki hii wawe wameshazilipa Benki fedha ambazo zinawadai za mwaka 2022-2023.
“Mameneja wote wa vyama kabla hamjaondoka Dodoma fedha za mwaka 2022 hadi 2023 muwe mmeshazilipa, na hili sio ombi ni lazima mzilipe fedha zao ili Fedha za benki zipatikane na mengine yaendelee.”
Naye Hamza Kitunga, Mwakilishi wa Wakulima Mkoa wa Tabora amesema Ucheleweshaji wa wakulima kutolipwa madeni yao yanawaathiri kwa kiwango kikubwa kwani hizo pesa ndizo wanazozitumia katika uzalishaji wa zao hilo la tumbaku.
“Kuchelewesha kwao malipo ya wakulima unatuathiri kwasababu baada ya manunuzi hayo na sisi lazima tununue pembejeo za kuweza kuzalisha tena zao, kwaio tunaomba wanunuzi walipe pesa zao kwa wakati,” amesema