Wakati kikosi cha Simba SC kikiendelea na maandalizi kuelekea mechi ya Mkondo wa Pili wa Robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly itakayopigwa Uwanja wa Cairo, Misri Ijumaa (Aprili 05), Kocha Mkuu wa timu hiyo Abdelhak Benchikha, ametaja mbinu zinazoweza kuwasaidia kupindua matokeo nchini humo, endapo wachezaji wataweza kuzitekeleza uwanjani.

Simba inakibarua kigumu cha kupindua matokeo ya bao 1-0, ililoruhusu ljumaa (Machi 29) katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, ambapo inatakiwa kupata ushindi zaidi ya huo ili kutimiza malengo yao ya kutinga Nusu Fainali ya michuano hiyo mikubwa zaidi kwa ngazi ya klabu Barani Afrika.

Akizungumza jijini Dar es salaam, Benchikha amesema mbinu pekee ya ushindi nchini Misri ljumaa (April 05) ni kuishambulia Al Ahly mfululizo kiasi cha kuwatia hofu, huku akitabiri utakuwa ni mchezo wa kupishana zaidi.

Kocha huyo amesema kama kwenye mechi ya kwanza hapa nchini walicheza kwa kujihami zaidi, lakini walifanikiwa kuingia ndani ya eneo lao la hatari zaidi ya mara saba, huku wachezaji wake wawikikosa mabao mengi, ana uhakika wanaweza kufanya zaidi ya mara hizo.

Kocha huyo amesema mfumo atakaocheza akiwa ugenini hautotofautiana na alioutumia ljumaa (Machi 29), ila kuna vitu ambavyo atawaongezea wachezaji wake ili kuwafanya wawe hatari zaidi wanapokuwa langoni.

Amesema kwa jinsi alivyoiangalia Al Ahly ni timu inayofikika kirahisi langoni mwao hata kama wanacheza kwa kujihami, na anaamini katika mechi ya marudiano hawatofanya hivyo, hivyo wataachia mianya mingi na nafasi.

“Hatuna cha kupoteza, tunaenda kushambulia Cairo, tutajaribu bahati yetu, inawezekana huko tutapata mabao, kwa nini isiwezekane?

“Mimi ni kocha na hii ni kazi yangu kwa miaka mingi, nimeshafundisha timu kubwa na zikacheza mechi kubwa zaidi kwa hiyo hata mechi hii ya marudiano tunacheza kwa ajili ya kushinda bila kuhofia chochote. Kama kufungwa tumeshafungwa, tutacheza kama fainali, ninachotaka na kuwaambia wachezaji wangu ni kwamba wapinzani wetu ndiyo wawe na hofu na sisi, na tukifanikiwa kupata bao na kulifuta lao la huku, mechi itakuwa nzuri zaidi,” amesema kocha huyo.

Kuhusu kuwa na dakika 90 ngumu Cairo kutokana na kucheza Ugenini mbele ya mashabiki lukuki wa Al Ahly, Benchika amesema timu kubwa kama Simba SC imeshakuwa moja kati ya zile zinazoogopwa Ugenini.

“Simba SC imeshatoka kwenye zile timu zinazohofia kucheza ugenini, tumeshacheza Cairo, Morocco, Algeria na tumecheza vizuri sana, tutacheza kama tulivyocheza mechi iliyopita, sasa wao ndiyo wataangalia wafanye nini, na kama wachezaji wangu watakuwa watulivu tukapata bao, mechi itakuwa ngumu kwao pia,” amesema

Katika mechi hiyo, Simba SC inahitaji ushindi kuanzia mabao 2-0 ama 2-1 au 3-2 na kuendelea ili kuweza kutinga Nusu Fainali, ambayo ndiyo malengo yao makuu msimu huu 2023/24.

Kocha Mashujaa auwekea mipango ukuta wake
Muundo wa NEMC kuwa Mamlaka washika kasi