Kocha Mkuu wa Mashujaa FC Mohamedi Abdallah “Baresi” amesema anaifanyia kazi safu ya ulinzi ya timu hiyo kupunguza makosa yanayosababisha mabao kwenye Ligi Kuu Soka Tanzania Bara.

Baresi amesemna ameamua kuivalia njuga safu yake ya ulinzi ili ipunguze makosa yanayosababisha waruhusu mabao kwenye michezo ya ligi na kusema wamedhamiria kufanya vizuri kwenye mechi zao zilizosalia lengo likiwa kubaki kwenye ligi hiyo.

“Licha ya timu yangu kufanya vizuri kwa kupata ushindi kwenye mechi za mzunguko wa pili bado timu yangu hasa kwenye eneo la ulinzi imekuwa ikifanya makosa mengi yanayosababisha mabao,” amesema Baresi aliyewahi pia kuinoa Mlandege ya Zanzibar.

Mashujaa wanashika nafasi ya 12 kwenye msimamo wa ligi wakiwa na pointi 21 katika mechi 21 ilizocheza, ikishinda mechi tano, sare sita, imefungwa mechi 10 wakifunga mabao 18 na kuruhusu wavu wao kuguswa mara 26.

Mashujaa wanajiandaa na mchezo wao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Coastal Union Aprili 12, Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma.

Aprili 16 watacheza na Azam, Uwanja wa Azam Complex, Dar es salaam, Aprili 28 watacheza na Young Africans Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma.

RUWASA yasambaza upendo wa Maji Kagera
Benchikha: Bado tuna nafasi Afrika