Manchester United imetuma maombi rasmi kwenda Klabu ya Southampton ya kumhitaji Jason Wilcox kuwa Mkurugenzi wa Michezo wa miamba hiyo ya Old Trafford.

Wilcox amewekwa kwenye kipaumbele cha Manchester United kushika wadhifa huo wa Mkurugenzi wa Michezo ikiwa ni mkakati wa klabu hiyo kuifanyia uboreshaji idara hiyo inayohusika na usajili wa wachezaji.

Mpango huo unaongozwa na mmiliki mwenza wa klabu hiyo, bilionea Jim Ratcliffe na kampuni yake ya INEOS.

Man United imetuma maombi rasmi yanayohusisha kulipa fidia kupata huduma ya winga huyo wa zamani wa Blackburn Rovers ingawa Southampton bado haijakubali mpango huo.

Southampton inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza haijafurahishwa na muda ambao Manchester United wametuma maombi hayo kwani wakati huu wanapambana kurejea Ligi Kuu.

Kocha Mkuu wa Southampton, Russell Martin alisema baada ya kipigo cha mabao 3-2 kutoka Ipswich juzi Jumatatu (Aprili Mosi) kuwa: “Ningeomba mnipe walau dakika 10 kutokana na matokeo ya kuhuzunisha ya usiku huu na tutachati wiki hii na nitakuwa na mengi ya kuwaambia”.

Aliongeza: “Sijazungumza na klabu kuhusiana na suala hilo. Mnajua hisia zangu kwa Jason, nitafanya mazungumzo naye baadaye.

Nina ujumbe wake akisema namna gani anajivunia kiwango kilichooneshwa na timu yetu. Mengine ni kama nilivyowaambia nitawajulisha baadaye”.

United inamhitaji Wilcox kabla ya dirisha kubwa la usajili la kiangazi.

Mpango wa klabu hiyo wa kumtaka Dan Ashworth kuwa Mkurugenzi wa Michezo umekwama baada ya Newcastle United kukataa kumuachia.

Naymar apanga kurudi nyumbani
Ancelotti: Real Madrid ina nafasi kubwa Ulaya