Shirikisho la Soka nchini Cameroon ‘FECAFOOT’ limemtangaza Marc Brys kuwa kocha mkuu wa timu ya soka ya taifa ya wanaume ya nchi hiyo ‘The Indomitable Lion’.
Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Michezo ya nchi hiyo, Brys kutoka Ubelgiji, anachukua nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa kocha wa timu hiyo Rigobert Song aliyemaliza mkataba wake.
Taarita hiyo imeeleza kuwa kwenye majukumu yake, Brys atasaidiwa na Joachim Munnga na Giannis Xilouris.
Pia wizara imewatangaza watu wengine kwenye benchi la ufundi, daktari wa timu na watu wa utawala.
Song aliyepewa jukumu la kuinoa Cameroon, Machi 2022, mkataba wake ulifikia kikomo Februari 29, mwaka huu.
Aliiongoza Cameroon kukata tiketi ya kushiriki Fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika Qatar mwaka 2022 na ingawa waliishia hatua makundi, alifanikiwa kuifunga timu ya taifa ya Brazil.
Kwenye Fainali za Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’ zilizofanyika Ivory Coast mwanzoni mwa mwaka huu, aliiongoza Cameroon kufika hatua ya l6 bora ambako walifungwa na Nigeria waliofika Fainali.
Song aliichezea timu ya taifa ya Cameroon michezo 137 akiwa kama nahodha wa timu hiyo kwa kipindi kirefu.