Kocha Mkuu wa Simba SC, Abdelhak Benchikha amesema jukumu la kufuzu Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika liko chini ya safu yake ya ushambuliaji.

Simba SC itakuwa wageni wa Al Ahly kwenye mchezo wa Mkondo wa Pili wa Robo Fainali utakaochezwa Uwanja wa Cairo International nchini Misri kesho Ijumaa (Aprili 05) ambao Wekundu wa Msimbazi watahitaji ushindi wa zaidi ya bao moja kuingia Nusu Fainali.

Benchikha amesema ameikabidhi safu ya ushambuliaji jukumu la kuwapeleka Nusu Fainali kwa kutumia vizuri kila nafasi itakayopatikana kwenye mchezo wa kesho Ijumaa (Aprili 05).

Kwenye mchezo uliofanyika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Ijumaa iliyopita (Machi 29) ambao Simba SC walifungwa bao 1-0, washambuliaji wa timu hiyo walipoteza nafasi za wazi za kufunga kitu ambacho kimesababisha kocha huyo kuwasisitiza juu ya jukumu hilo.

Benchikha amesema alitumia siku tano kuwapa mbinu na kuikumbusha safu ya ushambuliaji umakini wa kutumia nafasi zitakazopatikana katika mchezo huo, aliouita kuwa ni wa fainali kwao, kwani unabeba hatima yao kuingia hatua inayofuata.

“Tunahitaji kuwa na wachezaji wenye uwezo mkubwa kwa ajili ya kupata matokeo ya mechi kubwa, nina imani na kile nilichowapa katika uwanja wa mazoezi ndani ya siku tano tunaweza kufanya vizuri ugenini,” amesema Benchikha.

“Al Ahly ni timu kubwa hilo linajulikana wazi na ina wachezaji wenye uwezo mkubwa, nasi tunahitaji wachezaji wenye uwezo mkubwa katika kuendeleza ushindani. Tumeyafanyia kazi makosa tuliyofanya kwenye mchezo uliopita na ni matumaini yangu hayatajirudia kwenye mchezo huu,” ameongeza.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba SC, Salim Abdal lah Try Again’ amesema wao ni wawindaji na wameenda kushindana na kutafuta ushindi ugenini dhidi ya wenyeji wao Al Ahly.

Hersi: Timu ipo tayari kupambana Afrika Kusini
SIMULIZI: Siri kubwa niliyoibeba moyoni kuhusu Keki