Uongozi wa Mabingwa wa Soka wa Tanzania Bara, Young Africans umewatoa hofu mashabiki wa klabu hiyo kuwa tayari wamepata basi litakalotumiwa na timu hiyo kuelekea mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns, Uwanja wa Loftus Versfeld, Pretoria, Afrika Kusini kesho Ijumaa (Aprili 05).

Basi lililobeba kikosi cha Young Africans lililoandaliwa na wenyeji wa mchezo huo Mamelodi Sundowns liliharibika kilometa dhache kutoka Uwanja wa Ndege wa Oliver Tambo jijini Johannesburg, kwenda kwenye hoteli ambayo timu hiyo ingefikia na kuzusha taharuki miongoni mwa mashabiki wa timu hiyo.

Hata hivyo, kwa msaada wa balozi wa Tanzania wa Afrika Kusini na sehemu ya uongozi wa Young Africans uliotangulia Afrika Kusini walipata usafiri uliowapeleka hotelini tayari kwa maandalizi yao kuelekea mchezo huo.

Akizungumza kutoka Afrika Kusini Rais wa Young Africans, Hersi Said alimshukuru Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, James Bwana na sehemu ya uongozi wa timu hiyo uliotangulia kuweka mazingira sawa ya mchezo huo kutatua changamoto hiyo.

“Tuliingia juzi kutokea Dar es salaam na kupata mapokezi mazuri kutoka kwa balozi wetu wa Tazania ambaye yuko hapa na watendaji wake, lakini pia tulipokewa na Mamelodi Sundowns ambao ni wenyeji wetu hapa. Mapokezi yalikuwa mazuri kutokea Airport, hatukuchukua muda mrefu kufanya taratibu za uhamiaji, tukakuta magari yashaandaliwa,” ameeleza Hersi

“Dakika chache baada ya kuanza safari, gari lililokuwa limebeba wachezaji wetu lilipata hitilafu, lakini kwa msaada wa balozi tuliweza kupata usafiri mwingine uliotufikisha hotelini.”

Amesema wenyeji wao Mamelodi SundoWns wamewaandaliwa usafiri mwingine ambao kwa kanuni za Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’ hawawezi kulikataa ingawa wao kupitia Balozi wa Tanzania na kwa taratibu zao, wameandaa basi lao watakalotumia wakati wote watakapokuwa Afrika Kusini.

Kwa upande wake, Balozi Bwana amewaomba Watanzania wanaoishi Afrika Kusini na nchi jirani kujitokeza kwa wingi kuishangilia timu hiyo kwenye mchezo huo.

Young Africans itahitaji ushindi ama sare yoyote ya mabao kwenye mchezo huo wa kesho Ijumaa (Aprili 05) ili kufuzu kwa mara ya kwanza katika historia ya klabu hiyo hatua ya Nusu Fainali. Mechi ya kwanza ilimalizika kwa sare ya kutofungana.

DCEA yanasa zaidi ya kilo 54,000 Dawa za kulevya
Washambuliaji Simba SC wapewa kazi maalum