Nyota wa Young Africans wameahidi watacheza na kupambana ‘Kufa na Kupona’ ili kuhakikisha wanaiondoa Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini katika mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika yanayoendelea.

Mamelodi Sundowns itaikaribisha Young Africans katika mechi ya marudiano ya hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakayochezwa kesho Ijumaa (Aprili 05) kuanzia saa 3:00 usiku kwenye Uwanja wa Loftus Versfeld, Pretoria.

Akizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake, nahodha wa Young Africans, Bakari Mwamnyeto, amesema yeye na wenzake wanafahamu jukumu linalowakabili la kuwapa furaha Wanachama, Mashabiki wa Young Africans na Watanzania kwa ujumla, hivyo hawatofanya mzaha.

Mwamnyeto amesema wamejipanga kucheza katika kiwango cha juu ili kupata ushindi katika mechi hiyo ya ugenini.

“Wachezaji wote wapo katika morali ya juu, hata wale majeruhi wameshaanza mazoezi, kina Khalid Aucho wapo hapa, hali ya hewa ni nzuri, tukijiandaa vizuri tunaweza kubadilisha matokeo hapa hapa Afrika Kusini.”

“Na sisi kama wachezaji tumeshajipanga na kupeana majukumu tutafia uwanjani, kinachotupa jeuri ni pamoja na kupambana, kucheza kwa juhudi kubwa lakini nyuma yetu kuna sapoti kubwa ya mashabiki ambao wamesafiri kwa wingi kutoka nyumbani hadi huku na wengine tumewakuta huku huku,” amesema nahodha huyo.

Meneja wa Young Africans, Walter Harrison, amesema kikosi chao leo Alhamisi (Aprili 04) kinatarajiwa kufanya mazoezi yake kwenye Uwanja ambao itachezwa mechi hiyo, huku akiwa na imani wanakwenda kuandika historia.

“Kikosi kilikuwa kinafanya mazoezi siku zote tangu kilipowasili, lakini leo Alhamisi (Aprili 04), tutafanya mazoezi kwenye uwanja rasmi tutakaocheza, tuna imani tunakwenda kuandika historia siku ya ljumaa,” amesema meneja huyo.

Benchikha atamba kupindua matokeo Cairo
Watendaji wazembe TANESCO kuchukuliwa hatua