Klabu ya Brighton imetengeneza faida iliyoweka rekodi ya Pauni milioni 122.8 (sawa na Sh bilioni 415) katika mwaka wa fedha wa 2022-23, ukiwa msimu wenye mafanikio zaidi katika historia ya klabu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu ya England.
Kwa muibu wa takwimu, faida baada ya kodi iliongezeka kila mwaka kwa karibu Pauni milioni 100 (sawa na Sh bilioni 324) kutoka Pauni milioni 24 (sawa na Sh bilioni 77), huku mauzo yakipanda kwa asilimia 17.2 hadi rekodi ya Pauni milioni 204.5.
Brighton ilimaliza nafasi ya sita kwenye Ligi Kuu msimu wa 2022-23 na kufika Nusu Fainali ya Kombe la FA na pia ilitengeneza faida kubwa kutokana na mauzo ya baadhi ya wachezaji wake muhimu.
Kwenye taarifa yake klabu hiyo ilisema kuwa takwimu zinaweza kusaidia “maendeleo makubwa” zaidi kwenye matokeo ya uwanjani.
“Katika msimu tulioweka historia uwanjani tulichukua hatua kubwa mbele kalika lengo la muda mrefu la klabu la kuwa endelevu zaidi na kutomtegemea mmiliki wa klabu,” alisema Mtendaji Mkuu wa Brighton, Tony Bloom.
Rekodi ya faida ya Brighton inakuja wakati klabu zingine zimetangaza hasara katika msimu wa Ligi Kuu wa mwaka 2022-23 zikiwamo Aston Villa (Pauni milioni 120 sawa na Sh bilioni 389) na Chelsea (Pauni milioni 90 sawa na Sh bilioni 292).
Timu zingine zilizotengeneza hasara ni Leicester (Pauni milioni 89 sawa na Sh bilioni 289), Newcastle United (Pauni milioni 73 sawa na Sh bilioni 237), Nottingham Forest (Pauni milioni 52 sawa na Sh bilioni 168) na Wolves (Pauni milioni 67 sawa na Sh bilioni 217).
Sehemu kubwa ya mapato ya Brighton msimu wa mwaka 2022-23 ilitokana na uchezaji wao uwanjani na kuuza wachezaji wake.
Baadhi ya wachezaji wake iliyowauza ni kiungo wa Mali, Yves Bissouma, beki wa kushoto wa Hispania, Marc Cucurella, mshambuliaji wa Ubelgiji, Leandro Trossard na kiungo wa kati wa Argentina, Alexis Mac Allister waliingiza faida ya Pauni milioni 121.4 (sawa na Sh bilioni 393) katika uhamisho.