Aliyekuwa Spika wa Bunge la Afrika Kusini Nosiviwe Mapisa-Nqakula ameshtakiwa kwa makosa 12 ya rushwa na moja la utakatishaji fedha, baada ya kufikishwa Mahakamani kwa mara ya kwanza alipojisalimisha kituo cha polisi hii leo asubuhi.
Mwanasiasa huyo, anatuhumiwa kuomba hongo ili kutoa kandarasi wakati alipokuwa waziri wa ulinzi ingawa alikanusha kutenda kosa lolote akisema hana tabia ya kufanya uhalifu.
Mwendesha mashtaka, Bheki Manyathi aliiambia Mahakama ya Pretoria kulikuwa na ushahidi wa kutosha dhidi ya Bi Mapisa-Nqakula, ingawa hata hivyo aliachiliwa kwa dhamana.
Baada ya wiki kadhaa za uchunguzi, Bi Mapisa-Nqakula alijiuzulu hapo jana Aprili 3, 2024 huku akisema uamuzi wake hauhalalishi kwamba ni dalili za kutenda kosa akidai uzito wa suala hilo katika uchunguzi hawezi kumfanya aendelee na jukumu lake.
Mwezi uliopita, kitengo maalum cha polisi kilivamia nyumba yake Johannesburg kuhusiana na uchunguzi wa ufisadi na mama huyo (67), wa mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi alikua spika mwaka wa 2021 na kabla ya hapo alihudumu kama Waziri wa Ulinzi kwa miaka saba.