Kocha Mkuu wa Young Africans Miguel Gamondi amesema anakiamini kikosi chake kuwa kinaweza kufanya maajabu katika mchezo wa Mkondo wa Pili wa Robo Fainali, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns.
Young Africans watashuka kwenye dimba la Loftus Versfeld kucheza dhidi ya Mamelodi Sundowns ya huko, mchezo utaopigwa saa 3:00 usiku wa saa za Afrika Mashariki.
Kocha gamondi amesema kikosi chake kipo tayari kwa mchezo huo wa maamuzi na ameridhishwa na maandalizi mazuri walioyafanya, hivyo anaamini dakika 90 zitatoa matokeo ya kushangaza.
“Kikosi kimefanya vizuri sana kwenye mazoezi, na siku zote mimi ni muumini wa kuamini na kufanya kazi kwa bidii, kupambana na kujituma, nimeona mashabiki wengi wametoka Tanzania na wamekuja kuisapoti timu yao, nawapa hongera sana, hii itatoa chachu kwa wachezaji kupambana kwa bidii mno,” alisema Gamondi.
Young Africans pamoja na kwamba inahitaji ushindi ili iweze kutinga hatua ya Nusu Fainali, inahitaji pia sare yoyote ya mabao ili kuweza kuiondosha Mamelodi Sundowns mashindanoni, kwani itabebwa na bao la ugenini, huku yenyewe ikiwa haijaruhusu bao lolote ikicheza nyumbani.
Kanuni za ligi hiyo zinasema hakutokuwa na muda wa nyongeza timu zitakapomaliza kwa sare yoyote ile, badala yake itaangaliwa aliyeshinda bao la ugenini, au mabao mengi ugenini ili kupata mshindi na kama timu zote zitakuwa zimetoka sare zinazofanana nyumbani na ugenini, basi moja kwa moja zitakwenda kupigiana mikwaju ya Penati baada ya dakika 90 za mchezo.
Kanuni hiyo pia inasema hata timu ikishinda idadi ya mabao kama yale ambayo mpinzani wake ameshinda katika mechi ya kwanza, basi moja kwa moja watakwenda kwenye mikwaju ya Penati na si kuongeza dakika.
Kwa maana hiyo, Young Africans ilitoka suluhu tena ya bila kufungana na wapinzani wao, na Simba ikashinda bao 1-0 Cairo, basi mikwaju ya Penati itahusika.