Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amehimiza suala la nidhamu, maadili, uwajibikaji, uadilifu, mshikamano, umoja na upendo baina ya Viongozi na Watendaji wa Serikali katika kutenda haki kwa Wananchi.
Dkt. Mwinyi ameyasema hayo katika Kongamano la Kiimani kwa Viongozi na Watendaji Wakuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar lililoandaliwa na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais na kuratibiwa na Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar ukumbi wa Idrissa Abdul-Wakil Kikwajuni, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Amesema suala la nidhamu sio kwa Majeshi peke yake ni suala la utumishi wa umma na kusema, ili kuwepo uwajibikaji , maadili na nidhamu jambo kubwa ni kuwa na hofu ya Mungu na kuchunga ahadi zinazotolewa ili kutekeleza wajibu kwa uadilifu.
Rais Dkt. Mwinyi amesongeza kuwa, kongamano lijalo waalikwe Wenza wa viongozi na watendaji wa Serikali ili wapate kujifunza mada zinazotolewa na Masheikh na Wahadhiri huku akisisitiza kuwa kodi ndiyo inayoendesha Serikali kwa kutekeleza huduma mbalimbali za kkijamiina kwamba ulipaji wa kodi ni halali.