Mshambuliaji Karim Benzema amewajibu wanakosoa kiwango chake kwenye klabu ya Al Ittihad ya Ligi Kuu ya Saudi Arabia kwa kusema anahitaji msaada na kwamba hawezi kushinda mechi peke yake.
Mshindi huyo wa zamani wa tuzo ya mwanasoka bora wa mwaka wa dunia ni mmoja kati ya wachezaji wenye majina makubwa na aliamua kujiunga na Ligi Kuu ya Saudi Arabia wakati wa dirisha kubwa la usajili la msimu uliopita akitokea Real Madrid aliyoitumikia kwa miaka 14.
Hata hivyo nyota huyo wa kimataifa wa Ufaransa amefunga mabao tisa katika mechi 20 alizoichezea timu yake kwenye ligi msimu huu.
Al Ittihad mabingwa wa ligi hiyo wa msimu uliopita inashika nafasi ya nne kwenye msimamo.
Alipoulizwa baada ya sare ya bila kufungana dhidi ya Al Taawoun mwishoni mwa juma lililopita alisema kwa nini anashindwa kuonesha kiwango alichokuwanacho kwenye klabu ya Real Madrid.
Benzerma alisema: “Kwa sababu hatuchezi mchezo unaofanana na sichezi na wachezaji sawa na niliokuwa pamoja nao Real Madrid.
“Nahitaji msaada ndani ya kiwanja, siwezi kushinda mechi peke yangu. Nahitaji mchezaji mwingine anisaidie, nahitaji mambo mengi. Lakini ni tofauti, huu ni msimu wangu wa kwanza Saudia. Nina imani nitamaliza vizuri.”