Simba SC imeharibu rekodi flani iliyokuwa nayo kimataifa baada ya kupasuka nje ndani mbele ya Al Ahly ya Misri, jambo ambalo ni kama limempa hasira kocha wa timu hiyo, Abdelhak Benchikha ambaye fasta ametuma ripoti ya awali inayoshtua kwa mabosi wa klabu hiyo juu ya kutaka kukifumua kikosi hicho.

Kipigo cha bao 1-0 nyumbani na 2-0 ikiwa ugenini mwishoni mwa juma lililopita ikiwa ni mara ya kwanza kwa Al Ahly kuinyanyasa Simba SC kwa staili hiyo tangu mwaka 1985 na kumtibulia Benchikha kupoteza pia mechi mbili dhidi ya wapinzani wao, kwani haikuwahi kutokea kabla ya kuja Msimbazi.

Kikosi cha timu hiyo kilirejea alfajiri ya jana Jumapili (Aprili 07) kikitokea Cairo, Misri ilipong’oka katika mechi za Robo Fainali na Ofisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Imani Kajula amesema Simba SC imejifunza hatua kubwa na wanaenda kujipanga upya kwa msimu ujao.

Kajula amesema kuwa, Simba SC licha va kukwama kwa mara tano katika hatua ya Robo Fainali, lakini bado wataendelea kufanya maboresho ya timu yao ili warudi kwa nguvu kubwa.

“Kila hatua unajifunza kitu, tumeona wapi tumekwama, kuna eneo ambalo tunatakiwa kuendelea kulifanyia kazi ili tufike tunakotaka, tukubaliane Simba SC haiko mbali kufika inakotaka kufika,” amesema Kajula na kuongeza;

“Tutaendelea kufanya maboresho makubwa tukishirikiana na benchi letu la ufundi ambalo tunaona kazi yao bora kwa muda ambao wamekaa hapa, kwa sasa tunarudi kwenye mashindano ya ndani.”

 

NYOTA WATANO

Wakati Kajula akiyasema hayo taarifa za ndani ya Simba SC zinaeleza kuwa, ripoti ya awali ya kocha Benchikha tayari ipo mezani mwa mabosi wa timu hiyo ikiwa inahitaji mashine mpya tano kwa dirisha lijalo la usajili.

Kwa mujibu wa chanzo chetu cha kuaminika kutoka Simba SC ni kwamba, ripoti hiyo itahitaji beki mpya wa maana wa kulia na kushoto, watakaokuja kuwapunguzia uchovu wakongwe Shomari Kapombe na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ ambao kwa sasa ndio wamekuwa wakipata nafasi zaidi kwenye timu hiyo.

Tshabalala ndiye mchezaji aliyecheza dakika nyingi ndani ya kikosi hicho cha Simba SC katika Ligi ya Mabingwa akicheza michezo tisa akitumia dakika 810, wakati Kapombe amecheza jumla ya michezo 8 akitumia dakika 720.

Hata hivyo, katika nafasi hizo wapo mabeki wengine kama David Kameta ‘Duchu’ na Israel Mwenda ambao wanapata nafasi kidogo kutumika.

Mbali na mabeki hao pia ripoti hiyo inahitaji kiungo mchezeshaji, washambuliaji wawili, lakini mmoja akiwa na ubora wa kucheza kama kiungo mshambuliaji anayetumia mguu wa kushoto.

Katika eneo la kiungo mkabaji Simba SC ina nyota wanne ambao ni Mzamiru Yassin, Sadio Kanoute, Fabrice Ngoma, Abdallah Khamis na Babacar Sarr aliyeingia katika dirisha dogo sambamba na washambuliaji wawili Pa Omar Jobe na Freddy Michael walioshindwa kuwafurahisha mashabiki wa klabu hiyo tangu walipotua.

Eneo la kiungo cha ushambuliaji mbali na Clatous Chama, Edwin Balua, Ladack Chasambi, Saleh Kalabaka, Kidu Denis, Luis Miquissone na Saido Ntibazonkiza.

Taarifa zaidi zinasema kuwa, wakati kocha akipendekeza mashine mpya, lakini kuna wachezaji waliopo sasa kikosini wapo katika hatari ya kupigwa panga ili kuwapisha wenzao kutokana na kushindwa kuwa msaada kwa Benchikha aliyeipa USM Alger ya Algeria taji la Kombe la Shirikisho na CAF Super Cup kabla ya kutua Msimbazi mwishoni mwa Novemba mwaka jana.

“Amependekeza usajili wa wachezaji watano kwa nafasi hizo, hii ikiwa na maana ni lazima wengine wapungue kuweka uwiano sawa, kwani anataka msimu ujao kufanya mambo makubwa zaidi” kilisema chanzo hicho.

Simba SC kwa sasa inajiandaa kushuka uwanja kesho Jumanne (Aprili 09) kuvaana na Mashujaa katika mechi ya Kombe la Shirikisho la CRDB  hatua ya l6 Bora itakayopigwa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, mkoani Kigoma.

Mikel Arteta amfurahia Kai Havertz
Karim Benzema avunja ukimya Saudia