Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameitaka Menejimenti ya Wizara ya Madini kuhakikisha inachukua hatua za dhati katika kutatua changamoto ambazo zinawakabili Watumishi wa Wizara na kuzifanyia kazi ili kuongeza ufanisi katika kutekeleza majukumu yao.
Dkt. Kiruswa ameyasema hayo wakati akifunga Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Madini lililofanyika Mji wa Serikali Mtumba – Jijini Dodoma na kuongeza kuwa ni muhimu Menejimenti kukumbuka mara zote kuwa watumishi ndiyo hazina kuu ya kutekeleza, kusimamia na kuhakikisha malengo yaliyowekwa ya Wizara na Sekta ya Madini yanatimia.
Amesema, “ni vyema tukaijali hazina hiyo. Aidha, ni vema kwa Menejimenti ya Wizara kuchukua hatua katika kutatua changamoto ambazo zinalalamikiwa na Watumishi wa Wizara na kuzifanyia kazi. Ni matumaini yangu kuwa mtazingatia yale mliyoyapata katika Mkutano huu na nisisitize suala la uwajibikaji na uzingatiaji wa sheria na kanuni katika utekelezaji wa majukumu yetu.”
Aidha, Dkt. Kiruswa alisisitza kuhusu kutekeleza maelekezo aliyoyatoa Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde wakati wa ufunguzi wa Mkutano huo ili kuwezesha Maendeleo ya Sekta. Awali, Waziri Mavunde alisisitiza kuongeza ubunifu na kwamba milango yake iko wazi kwa Watumishi kumshauri kwa manufaa ya Wizara na Sekta ya Madini.
Kwa upande wake Mweyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Madini na Naibu Katibu Mkuu, Msafiri Mbibo alisema Wizara itaendelea kuboresha mazingira ya kazi kwa Watumishi huku akiahidi kuwa Menejimenti itafanyia kazi maelekezo ya Waziri kuhusu kusikiliza na kutatua changamoto za Wafanyakazi sambamba na kuendelea kuwajengea uwezo ili kuongeza ufanisi katika kutekeleza majukumu yao.