Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Abas Mtemvu amewaongoza Viongozi na Wana CCM kukabidhi Msaada wa mahitaji ya chakula na vifaa kwa Waathirika wa mafuriko katika kata 12 za Wilaya ya Rufiji Mkoani Pwani.
Akizungumza wakati wa kukabithi msaada huo wenye thamani ya zaidi ya milioni 22 kwa Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Meja Edward Gowele katika Shule ya Msingi Umwe Ikwiriri amesema, msaada huo ni utekelezaji wa ahadi aliyotoa wiki iliyopita mbele ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa, Abdulamani Kinana.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Rufiji Meja Edward Gowele alishukuru kwa msaada huo kutoka kwa Wana CCM, Wananchi na Wadau wa Mkoa wa Dar es Salaam na kusema zoezi la kuhamisha Wananchi mashambani bado litaendelea, ili kupisha mafuriko hayo.
Amesema tayari uongozi wa Wilaya hiyo umetenga viwanja zaidi ya 600 kwa ajili ya Wananchi waliokumbwa na mafuliko hayo na kusema eneo hilo ni salama halitakuja kufikiwa na mafuriko.
Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ubungo, Rogart Mbowe alisema Mtemvu baada ya kutoka Rufiji katika ziara y Kinana aliwaagiza wenyeviti wa CCM Wilaya za Mkoa wake watafute misaada hiyo, ili kuifikisha kwa ndugu zao wa Wilaya ya Rufiji walioathiriwa na mafuriko hao.
Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya AMO foundation. Amina saidi ambaye alichangia misaada hiyo zaidi ya tani kumi za unga wa sembe amezitaka Taasisi na mashirika yasiyo ya kiserikali kupeleka misaada yao ya hali na Mali kwa waathirika hao wa mafuriko ya Wilaya ya Rufiji.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Dar es Salaam, Hadija Ally Saidi alisema vyakula zaidi ya tani 13 vilivyoletwa ni Mchele , Maharage, Unga wa Sembe, Maji ya kunywa, magodoro 100.
Akishukuru kwa msaada huo, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Rufiji, Kaswakala Mbonde alisema mafuriko hayo yana historia ya zaidi ya mia 50, hivyo amewataka Watanzania kutokubali kupotoshwa kwamba ni athari za Bwawa la kuzalisha Umeme la Mwalimu Julius Nyerere.