Afarah Suleiman, Babati – Manyara.
Mahakama kuu Kanda ya Manyara imefutilia mbali rufaa ya Hashimu Ally, dhidi ya Mbunge wa jimbo la Babati Mjini, Pauline Gekul kwa madai kuwa imekosa na mashiko.
Maamuzi hayo, yametolewa na Jaji wa Mahakama hiyo, Devotha Kamzora huku akiwataka warufani kukata upya rufaa kama hawajaridhika na maamuzi hayo.
Kwa upande wake wakili wa Hashimu Ally, Peter Madeleka amesema hajaridhishwa na maamuzi hayo kwani kuna madudu yanaendelea kwenye kesi hiyo, hivyo ndani ya siku mbili watahakikisha wanakata rufaa, ili haki dhidi ya mteja wake itendeke.
Naye wakili wa Pauline Gekul, Efraim Kisanga amesema maamuzi yaliyotolewa na Jaji Devotha ni sahihi, hivyo muda wowote kuanzia sasa mteja wake atafungua kesi ya madai kwa wale wote waliomchafua kupitia kashfa hiyo na ukweli wote utajulikana ndani ya muda mfupi.
Pauline Gekul, alifikishwa Mahakama ya Wilaya ya Babati akikabiliwa na kesi ya jinai namba 577 ya mwaka 2023, kwa kosa la kumuingizia chupa kinyume na maumbile aliyekua Mfanyakazi wake, Hashimu Ally, kesi ambayo ilitupitiliwa mbali na Mkurugenzi wa Mashtaka kutokana na mamlaka aliyopewa.
Hata hivyo, hii inakuwa ni mara ya pili kwa Mbunge huyo Pauline Gekul kushinda kesi hiyo, licha ya mrufani wake kutaka kukata rufaa Mahakamani hapo.