Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Mahakama zimeanza kutumia mfumo unaonasa sauti na kuzibadilisha kwenda kwenye maandishi huku ukitafsiri lugha za Kiingereza na Kiswahili.
Majaliwa ameyasema hayo Bungeni, jijini Dodoma wakati akitoa hoja ya kuhitimisha mjadala wa bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2024/2025.
Amesema, “hii ni hatua kubwa sana kwani mfumo huo unarekodi sauti na kupeleka kwenye maandishi. Vilevile, unaweza kutafsiri lugha ya Kiswahili au Kiingereza kulingana na uhitaji. Kanuni za Mahakama zimeanza kutafsiriwa sambamba na uandaaji wa mihutasari ya hukumu kwa Kiswahili ili kuwawezesha wananchi kuelewa mwenendo wa mashauri.”
Majaliwa amesema mbali ya matumizi ya Kiswahili Mahakamani, Serikali imeendelea kuimarisha matumizi ya TEHAMA ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia kutokana na mapinduzi ya nne ya viwanda duniani.
“Jitihada hizo zimeanza kuleta mafanikio katika utendaji wa Serikali kwa kuunganisha Serikali yote (Wizara, Idara, Wakala na Taasisi zake) ziweze kusomana kimfumo. Tumeanza kupata mafanikio mfano: Mahakama ya Tanzania, ambapo mifumo mbalimbali ya TEHAMA imejengwa ili kurahisisha na kuharakisha utoaji wa haki kwa wananchi,” ameongeza Majaliwa.
Ameitaja mifumo hiyo kuwa ni pamoja na Mfumo wa Usajili, Uendeshaji na Usimamizi wa Mashauri kwa ajili ya kurahisisha, kuharakisha na kuokoa muda wa mwenendo wa mashauri mahakamani.