Aina ya Chanjo za Magonjwa ya Mifugo zilizozalishwa na Taasisi ya Kuzalisha Chanjo Tanzania – TVI, iliyopo mjini Kibaha, zimefika saba huku Serikali ikitoa kiasi cha shilingiBil. 51.66 kwa ajili ya kuimarisha miundombinu mbalimbali katika Sekta ya Mifugo.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Aprili 16, 2024, Waziri wa mifugo na uvuvi, Abdallah Ulega amesema Chanjo hizo ni zile za Mdondo kwa Kuku, Kimeta kwa Ng’ombe, Mbuzi na Kondoo, Chambavu kwa Ng’ombe, Mbuzi na Kondoo.
Amesema, “lakini pia Chanjo mchanganyiko wa Kimeta na Chambavu,ugonjwa wa Kutupa Mimba kwa ng’ombe, Homa ya Mapafu ya ng’ombe na Homa ya Mapafu ya mbuzi, chanjo mbili mpya za Kichaa cha Mbwa na Sotoka ya Mbuzi na Kondoo ziko katika hatua za awali za utengenezaji.”
Ulega ameongeza kuwa, idadi ya dozi za chanjo zinazozalishwa kwa mwaka imeongezeka kutoka dozi milioni 11.5 mwaka 2012/2013 hadi kufikia dozi milioni 63.6 mwaka 2020/2021 na kwamba chanjo hizo zimepunguza vifo vya mifugo na hivyo kuihakikishia jamii kupata chakula na protini itokanayo na wanyama hususani Ngombe, muzi kondoo na kuku.
“Na Miundombinu iliyoimarishwa inajumuisha Ujenzi wa miundombinu ya minada ya mifugo ya kisasa 51 shilingi bilioni 17.5 Ujenzi wa Majosho 746 kwa gharama ya shilingi bilioni 15.92 katika Halmashauri mbalimbali nchini na kuchangia kuongezeka kwa idadi ya mifugo inayoogeshwa, kupunguza magonjwa ya mifugo yaenezwayo na kupe kutoka asilima 72 hadi asilimia 48,Ujenzi wa Vituo 10 vya kukusanyia Maziwa kwa shilingi bilioni 2.5,ujenzi wa Mabwawa 15 kwa shilingi bilioni 8.04 kwenye Halmashauri mbalimbali nchini,” amesema Ulega
Ameongeza kuwa, “uzalishaji wa kuku na mayai ya kutosha umekuwa na faida kwa pande zote mbili za muungano, kwa mfano kupata chakula kwa ajili ya hoteli za kitaalii zilizoko Zanzibar na Tanzania bara.”