Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Ali Bagheri Kani ameionya Israel kutofanya kosa jipya, kauli inayokuja ikiwa ni muda mchache baada ya Mkuu wa Majeshi ya Israel, Luten Generali Herzi Halevi kuapa kuchukua hatua za kulipiza kisasi kutokana na shambulizi la Iran kwa Israel Aprili 14, 2024.
Kani amesema safari hii Iran itajibu kosa la Israel kwa vitendo “ndani ya sekunde chache, kauli ambayo inaonekana kuchochea mgogoro huo, kwani bila ya kutoa maelezo, Luteni Jenerali huyo wa Israel, Halevi alisema shambulio la Iran litajibiwa.
Mapema hapo jana Aprili 15, 2024 Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za nje ya Ujerumani, alisema nchi hiyo imemuita Balozi wa Iran, kufuatia mashambulizi yaliyofanywa na Tehran dhidi ya Tel Aviv huku Iran ikisema hatua iliyochukuliwa inaonesha misimamo isiyowajibika ya Ujerumani, Ufaransa na Uingereza ambazo zote zimewaita mabalozi wa Iran katika nchi zao kujadili shambulio hilo.
Kwa mara ya kwanza katika historia, Iran ilimshambulia moja kwa moja adui yake wa miaka mingi Israel kwa droni zaidi ya 300 pamoja na kufyatua makombora yaliyofanikiwa kudunguliwa kwa asilimia 99, ikijibu shambulizi linalodaiwa kufanywa na Israel katika ubalozi wake mdogo nchini Syria, lililosababisha mauaji ya makamanda wake.