Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amefunga Maonesho ya Wiki ya Nishati katika Viwanja vya Bunge jijini Dodoma huku akitoa maagizo kwa Wizara ya Nishati na Taasisi zake kuendelea kuboresha maonesho hayo na utoaji wa huduma kwa Wananchi.

Akizungumza hii leo jijini Dodoma katika kilele cha maonesho hayo, ameitaka Wizara ya Nishati kuweka mkakati wa kuhakikisha yanakuwa endelevu, ili wabunge wapate fursa za kuwasilisha hoja zao moja kwa moja kwa wataalam na kupewa majawabu ya hoja na changamoto zinazowakabili wao na Wananchi wanaowakilishwa.

Aidha, ameagiza Maonesho ya Nishati yafanyike kuanzia ngazi ya Wilaya, Mikoa na Halmashauri, ili yale yanayofanyika Makao Makuu yabaki kuwa ya Kitaifa.

“Kwa kufanya hivyo, huduma zitakuwa zimesogezwa zaidi kwa Wananchi na pia Mameneja wa TANESCO wa Kanda, Mikoa na Wilaya toeni ufafanuzi wa hoja na changamoto zinazowakabili Wananchi,”amesema.

Aidha Majaliwa ameongeza kuwa, “na Wizara mnapaswa kuweka mkakati wa kuwawezesha wananchi wote kupata ufafanuzi na fursa zinazotokana na miradi inayotekelezwa katika Sekta ya Nishati.”

Hata hivyo, ameagiza maonesho hayo yafanyike maeneo yanayofikika kwa urahisi kwa wananchi wengi kama vile katikati ya miji ili wananchi wengi washiriki na kupata ufafanuzi wa masuala mbalimbali.

Naye Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati,  Dkt. Doto Biteko amelipongeza Shirika la Umeme – TANESCO, kwa kuendelea kuboresha utoaji wa huduma ya umeme nchini.

“Tunafanyakazi kubwa kubadilisha taswira ya Wizara ya Nishati na Taasisi zake na niwashukuru sana watendaji wa Wizara hii na Taasisi zake kwa kufanyakazi kwa juhudi na niwaombe waongeze kasi,” alisema.

“Na niwapongeze Wakandarasi wa umeme kwa kuendelea na utekelezaji wa miradi ya nishati katika maeneo mbalimbali nchini Lakini pia nipongeze Vyombo vya Habari kwa kuendelea kutangaza Habari zinazohusu masuala ya nishati kwa lengo la kujibu hoja na maswali mbalimbali ya wananchi,” amesema Dkt. Biteko.

Katabazi: Viongozi wa dini kemeeni ukatili wa kijinsia
Watakiwa kusimamia miradi ya maendeleo kwa ufanisi