Michuano ya CECAFA Senior Chalenji ambayo kwa mwaka huu yatafanyika Visiwani Zanzibar, yamesogezwa mbele hadi Julai 6, badala ya Juni 29, tarehe iliyopangwa hapo awali.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Zanzibar ‘ZFF’, Hussein Ahmada Vuai, amesema kusogezwa mbele kwa mashindano hayo kumetokana na sababu ambazo zipo nje ya uwezo wao, ikiwamo ombi la wadhamini ambao wameomba kufanyika mwezi huo.
Amesema matarajio yao katika mashindano hayo ni kuwapo kwa ushindani mkali kwa nchi shiriki, ambapo sasa yataanza Julai 6 hadi 21, mwaka huu.
Vuai amesema maandalizi yanakwenda vizuri na tayari timu ya CECAFA ambayo walikuwa na ukaguzi wa miundombinu kwa ujumla wake kwa ajili ya mashindano ya shule kwa vijana walipata nafasi hiyo ya kukagua miundombinu yote ya Zanzibar kwa hatua ya awali.
Aidha, amesema timu hiyo ya ukaguzi, inatarajiwa kuja tena kufanya ukaguzi huo kutokana na taratibu zao, ingawa wameridhishwa na hali ya miundombinu ya hapa nchini.
“Wazanzibari wajiandae mashindano yapo na tunatarajia ukaguzi wa awamu ya pili ambao ndio wa mwisho utakaofanyika ndani ya mwezi ujao, lakini tunaamini kila kitu kinakwenda vizuri,” amesema.
Hata hivyo, amesema mpaka sasa wamekuwa na ushirikiano mzuri na wanajiandaa vyema kuhakikisha mashindano hayo yanafanikiwa.