Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya – DCEA, imefanya operesheni na kufanikiwa kukamata jumla ya kilo 767.2 za dawa za kulevya katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Tanga katika kipindi cha wiki mbili kuanzia Aprili 4 hadi 18, 2024.
Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, ametangaza mafanikio hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa Habari hii leo Aprili 22, 2024, jijini Dar es Salaam na kusema aina ya dawa zilizokamatwa ni pamoja na heroin (kilo 233.2), methamphetamini (kilo 525.67) na skanka (kilo 8.33) ambapo watu 21 wamekamtwa.
Amezitaja operesheni zilizofanikisha ukamataji wa dawa hizo kuwa ni ilizofanyika jijini Tanga eneo la Mikanjuni tarehe 4 Aprili,2024 ambapo watuhumiwa wawili walikamatwa na gramu 329.412 za heroin, iliyofanyika eneo la Wailes Temeke mtaa wa Jeshini jijini Dar es Salaam Aprili 8, 2024.
Katika operesheni hiyo walifanikisha kuwakamatwa watuhumiwa wawili na kilogramu 1.49 za skanka, iliyofanyika eneo la Zinga Bagamoyo mkoani Pwani Aprili 10, 2024 na kufanikisha kuwakamata watuhumiwa watatu wakiwa na kilogramu 424.84 za dawa ya kulevya aina ya Methamphetamine. Pia mtuhumiwa mwingine mmoja alikamatwa na gramu 158.24 za heroin eneo la Kunduchi jijini Dar es Salaam tarehe 10 Aprili.
Amesema, “aidha, tarehe 14 Aprili, 2024 tulifanya operesheni katika eneo la bandari jijini Dar es Salaam na kufanikiwa kukamata kilogramu 4.72 za dawa za kulevya aina ya skanka pamoja na kuwakamata watuhumiwa watatu kuhusika na dawa hizo.”
“Vilevile, tarehe 16 Aprili, 2024 tuliendelea na operesheni jijini Dar es Salaam, katika kata ya Kunduchi na kukamata kilogramu 232.69 za dawa za kulevya aina ya heroin na kilogramu 100.83 za dawa ya kulevya aina ya methamphetamine zilizokuwa zinaingizwa nchini kupitia Bahari ya Hindi. Watuhumiwa waliokamatwa katika tukio hilo ni tisa,” amesema Lyimo.
Pia amefichua mbinu mpya ya ufichaji wa dawa za kulevya inayotumiwa na wafanyabiashara wa dawa za kulevya kusafirisha dawa hizo haramu. Ameeleza kuwa baadhi ya dawa zilizokamatwa zilikuwa zimefichwa kwa ustadi kwenye vifungashio vilivyoandikwa majina ya kahawa na chai ili kukwepa kukamatwa.