Kinjekitile “Bokelo” Ngwale ni jina maarufu zaidi katika historia ya Tanzania na ni vigumu kuizungumzia Historia ya vita vya Majimaji pasipo kumtaja Shujaa huyu ambaye alizaliwa Ngarambe Umatumbini ingawa tarehe, Mwezi na Mwaka aliozaliwa bado havijawekwa katika kumbukumbu sahihi.
Mwanzoni mwa karne ya 20 aliwashawishi watu katika Ukanda wa Kusini ya Tanzania kusimama kidete na kupambana dhidi ya mtutu wa bunduki wa Wajerumani waliokuwa wakiitawala Tanganyika wakati wa ukoloni, akiwaahidi kuwalinda kwa maji ya miujiza.
Kinjekitile anachukuliwa kama ishara ya upinzani dhidi ya utawala wa kikoloni wa Ujerumani nchini Tanzania, akidai kwamba yeye ni roho na kuwataka watu wa Tanganyika kuwapinga Wakoloni ambapo aliwapa maji aliyodai kuwa na dawa ambayo yangewafanya wasiweze kudhurika.
Alisema Dawa hiyo alipewa na Bokelo au Mungu, akidai kwamba mtu huyo ni roho aliyejitokeza kwake katika umbile la nyoka, akamburuza Kinjeketile chini ya maji kwa saa ishirini na nne, alipoibuka alikuwa amekauka na akaanza kufanya utabiri.
Kinjekitile anafahamika pia kwa kuyaunganisha makabila ya eneo hilo na kadri ujumbe wake ulivyozidi kusambaa, akachangia kuwa mtu wa kwanza kuleta utaifa katika ardhi ya Tanganyika na alijulikana zaidi pale alipowaambia wafuasi wake iwapo watatumia maji yake yaliyo na dawa, risasi za Wajerumani hazingewaingia yaani zingeyeyuka.
Ni mwanzilishi wa vita vya Maji Maji, ingawa yeye mwenyewe alikufa kwa kunyongwa muda mfupi baada ya vuguvugu hilo kuanza, ikikumbukwa kuwa kati ya mwaka 1905 na 1907 Vita hivyo vilishika kasi na vilikuwa mojawapo ya vita vikuu dhidi ya ukoloni barani Afrika.
Inakadiriwa kwamba kati ya watu 180,000 hadi 300,000 walifariki dunia wakati wa vita hivyo huku sababu nyinginezo kama njaa na magonjwa zikichagiza zaidi na aliwaambia watu wake risasi zitakapopigwa wawe wanatamka neno Majiiiii kisha zitabadilika na kuwa maji.
Hata hivyo, alinyongwa mwezi Agosti mwaka 1905 na maafisa wa Ujerumani kwa kosa la uchochezi.