Klabu ya Liverpool inaamini katika uwezo wa Mshambuliaji wa Juventus Federico Chiesa na huenda ikaingia katika mpango wa kumsajili, endapo Mshambuliaji wao kutoka nchini Misri Mohamed Salah, ataondoka mwishoni mwa msimu huu.
Salah amekuwa akihusishwa na mpango wa kutaka kuhamia Saudi Arabia, na tayari klabu kadhaa zinazoshiriki Ligi Kuu nchini humo ‘Saudi Pro League’ zinatajwa kumuwania Mshambuliaji huyo, ambaye amekuwa muhimili mkubwa katika safu ya Ushambuliaji ya Liverpool.
Hadi sasa Chiesa mwenye umri wa miaka 26, amefunga mabao manane na kutoa pasi mbili za mabao katika michezo 30 aliyocheza msimu huu 2023/24.
Ripoti nchini Italia zimedai kwamba, Liverpool wanaweza kufufua hamu yao ya kumsajili Mshambuliaji huyo wakati wa usajili wa msimu wa joto.
Mkataba wa sasa wa Mshambuliaji huyo kutoka nchini Italia unamalizika msimu ujao wa joto huku Tuttosport ikidai kuwa Liverpool inaweza kumpata kwa urahisi.
Inadaiwa kuwa klabu ya Juventus inayoshiriki Ligi ya Serie A kwa sasa iko kwenye mazungumzo na Chiesa kuhusu uwezekano wa kumsainisha mkataba mpya na ikiharakisha kufikia makubaliano kabla ya michuano ya Uropa msimu huu 2023/24.
Iwapo Chiesa atashindwa kukubaliana na mpango wa kusaini mkataba mpya klabuni hapo, Liverpool watakuwa na nguvu ya kumsajili kama mbadala wa Mohamed Salah, ikiwa Mshambuliaji huyo ataaamua kuondoka Merseyside.