Matumizi ya kijeshi yameongezeka Duniani yameongezeka kwa asilimia 7 kutokana na kuzorota kwa amani na usalama, huku nchi kumi zilizokuwa na matumizi makubwa ya kijeshi kwa mwaka 2023 zikiongozwa na Marekani, China na Urusi.
Hayo yamebainishwa na Taasisi ya kimataifa ya utafiti wa masuala ya amani na usalama – SIPRI ya jijini Stockholm Nchini Sweden kupitia Mtafiti wake Mkuu katika mpango wa uangalizi wa matumizi ya kijeshi na utengenezaji wa silaha Nan Tian.
Amesema, mataifa yamekuwa yakiweka mbele nguvu za kijeshi na matokeo yake ni kuhatarisha usalama wa duniaikitolea mfano taifa la Urusiambalo limeongeza matumizi yake kwa asilimia 24, Ukraine kwa asilimia 51 inayopokea angalau dola bilioni 35 za msaada wa kijeshi kutoka kwa Mataifa ya Magharibi.
“Nchi wanachama wa Jumuiya ya kujihami ya NATO zimetumia takriban asilimia 55 ya matumizi ya kijeshi duniani, miaka miwili ya vita vya Urusi nchini Ukraine imebadilisha kabisa muonekano wa usalama na kutoa kitisho zaidi cha usalama badala ya amani na uthabiti duniani,” amesema Tian.
Katika Mataifa ya Afrika, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo iliongeza matumizi yake kwa asilimia 105, kutokana na mgogoro unaoendelea kati ya serikali na makundi yaliojihami ya waasi na kwamba migogoro ya kikanda na uboreshaji wa kijeshi pia ni miongoni mwa sababu.
Hata hivyo, SIPRI inasema katika utafiti watakaoufanya mwaka 2024 matumizi ya kijeshi huenda yakaongezeka zaidi kufuatia shambulizi la Israel dhidi ya wanamgambo wa Hamas la ukanda wa Gaza na wasiwasi uliopo wa mzozo wa kanda nzima ya Mashariki ya Kati.