Beki kutoka nchini Brazil na Klabu ya Arsenal Gabriel dos Santos Magalhães, amesema kuna mambo makubwa yanakuja kwa The Gunners ikiwa wanaweza kumaliza msimu huu kwa kushinda michezo yao yote iliyosalia, huku akijadili jinsi safu ya ulinzi ya klabu hiyo ilivyoimarika.

Kabla ya mpambano wao mkali wa London daby dhidi ya Chelsea utakaopigwa baadae leo Jumanne (Aprili 23), Kikosi cha wa Mikel Arteta kipo kileleni mwa msimamo wa Ligi ya England kikiwa na alama 74 sawa na Liverpool, huku Manchester City ikiwa na alama 73 na mchezo mmoja mkononi.

Arsenal wanaingia katika hatua ya mwisho msimu huu wakiwa na matumaini ya kupata mwenendo mzuri wa matokeo, jambo ambalo halikuwa hivyo msimu uliopita, kwani Beki William Saliba aliumia wakati wa mchezo wa Ligi ya Barani Ulaya ‘UEFA Europa League’ dhidi ya Sporting Lisbon ya Ureno, mnamo Machi 16 mwaka jana.

Beki huyo kutoka nchini Ufaransa hakuonekana tena kwenye Michezo ya Ligi Kuu, hali ambayo ilipunguza ukali wa safu ya Ulinzi ya Arsenal na kuipa nafasi Man City kutwaa taji lao la tano ndani ya miaka sita.

Kutokana na utofauti wa msimu uliopita na msimu huu, Beki Gabriel amesema ni hatua nzuri kwa Arsenal kuendelea kuwa na Beki kama Saliba hadi sasa, kwani anaamini uwepo wake umeongeza kitu kwenye kikosi chao ambacho msimu huu kinapambana kurudisha heshima ya ubingwa iliyopotea miaka 20 iliyoipita.

Gabriel amesema: “Ilikuwa ngumu kwetu kwa sababu tulikuwa tunacheza kila mechi pamoja, na bila shaka mambo hubadilika wachezaji wengine wanapoingia.

“Kwa mfano Jakub Kiwior aliingia, ni beki wa kushoto na aliingia upande wa kulia. Ilikuwa ngumu kwake, lakini hiyo imepita sasa.

“Tunajua tuko vizuri na lazima tuendelee hivyo hivyo. Tumebakiza mechi tano katika ligi na lazima tuendelee pamoja msimu mzima, kwa sababu kama tutashinda mechi hizo tano, kuna mambo makubwa yanakuja.”

“Msimu uliopita ulikuwa mzuri, katika michezo wa tuliyocheza pamoja. Tayari tunaelewana vizuri uwanjani,” Gabriel alisema kuhusu mlinzi mwenzake kutoka nchini Ufaransa Saliba.

“Mwaka huu nilikuwa na uhakika kwamba tukiwa na watu pamoja itakwenda vizuri zaidi, kwa sababu tunafanya kazi nyingi, tunazungumza sana, kwa hiyo hiyo inatusaidia.

“Nadhani mwaka huu, pia tuna imani kubwa. Kila mmoja wetu ana imani na mwenzake, anajiamini kwa mchezaji yeyote anayecheza. Kwa hivyo hiyo ni nzuri kwetu.”

Akitafakari jinsi safu yao ya nyuma ilivyofikia kiwango hicho, Gabriel aliendelea: “Msimu uliopita tayari tulikuwa wazuri. William aliumia, lakini tulikuwa wazuri na tulizungumza mengi kati yetu.

“Mwaka huu tuko vizuri hata kama tutabadilisha beki wetu wa kushoto au nafasi nyingine.

“Nadhani pia kumekuwa na kazi nyingi, kila kitu tunachofanyia kazi ni kwa ajili ya kulinda vyema. Tunapocheza pamoja sana, tunaelewana zaidi na hilo limetusaidia vyema.”

“Kumekuwa na mambo mengine katika uboreshaji wa safu ya ulinzi pia, kuwasili kwa Declan Rice majira ya joto yaliyopita kuathiri vyema nguvu ya timu, uimara na aina mbalimbali.” Amesema Gabriel

Prof. Mkenda: Walioathiriwa na mafuriko wapokelewe bila masharti
Wachimbaji Wadogo wamuamsha Waitara Bungeni