Uzalishaji wa umeme kupitia mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maji wa Julius Nyerere (JNHPP) wenye uwezo wa kuzalisha Megawati 2,115, ambapo uzalishaji huo umeanza kwa Megawati 235 kupitia mtambo namba tisa umeanza.
Hayo yamesema na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko Bungeni jijini Dodoma wakati akisoma hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Nishati kwa mwaka wa fedha 2024/2025 na kuongeza kuwa, “matarajio ni mradi huu kukamilika Desemba 2024 kwa mitambo yote nane yenye uwezo wa kuzalisha Megawati 235 kila moja kuwa inazalisha umeme.”
Amesema, Wizara imepanga kukamilisha mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia mradi wa Julius Nyerere (MW 2,115) ambapo kazi zilizopangwa kutekelezwa ni pamoja na kukamilisha ujenzi wa jengo la mitambo (power house) na ufungaji wa mitambo saba (7) ya kuzalisha umeme ambayo kwa sasa ipo katika hatua mbalimbali za ukamilishwaji.
“Wizara pia itaendelea na utekelezaji wa mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia wa Kinyerezi kwa kukamilisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 132 yenye urefu wa kilomita 19.2 kutoka kituo cha kuzalisha umeme cha Kinyerezi kwenda Gongolamboto hadi Mbagala Jijini Dar es Salaam na kufunga transfoma maeneo ya Gongolamboto na Mbagala,” amebainisha Dkt. Biteko.
Miradi mingine ya uzalishaji wa umeme itakayotekelezwa ni mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maji wa Malagarasi – MW 49.5; mradi wa kuzalisha umeme jua Shinyanga – MW 150; ukarabati wa mitambo ya kuzalisha umeme katika Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Hale; mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maji wa Kakono – MW 87.8; na mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maji ya mto Kikonge–MW 321.
Aidha, Serikali pia itaendelea kuelekeza nguvu katika uzalishaji wa umeme jotoardhi ambapo itakamilisha uchorongaji wa visima vitatu (3) vya uhakiki (exploratory wells) ili kuhakiki hifadhi, kiwango na ubora wa rasilimali ya jotoardhi katika mradi wa Ngozi (Mbeya) wenye uwezo wa kuzalisha MW 30 kwa awamu ya kwanza pamoja na kuanza ujenzi wa mtambo mdogo wa kuzalisha umeme (wellhead generator) wa MW 5.