Kigezo cha ziada ya kuzipima Halmashauri zote nchini kuanzia mwaka wa fedha ujao ni kila Halmashauri kubuni vyanzo vipya vya mapato kuanzia viwili na kuendelea kwa kila mwaka wa fedha, huku viongozi wa Halmashauri zote nchini kuzingatia matumizi ya mifumo katika shughuli zote za utumishi, manunuzi na ukusanyaji wa mapato.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa amesema wakati wa kufungua Mkutano wa 38 wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa – ALAT Taifa unaofanyika Zanzibar na kuongeza kuwa, nguvu ya kila Halmashauri ni mapato na ili iweze kutekeleza miradi yenye tija lazima kuwe na mapato ya uhakika.
Amesema, “hili tulishalijadili na kamati tendaji ya ALAT na kukubaliana sasa kuanzia mwaka ujao wa fedha kigezo hili kitaingizwa rasmi katika vigezo vya upimaji wa utendaji kazi kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa.”
Aidha, Mchengerwa alizitaka Halmashauri zote nchini kuhakikisha zinafanya makadirio ya ukusanyaji wa mapato kwa kuzingatia takwimu sahihi za vyanzo vya mapato hivyo kila Halmashauri ina wajibu wa kufanya tathmini ya vyanzo vyake na kubajeti kwa kuzingatia takwimu sahihi.
“Hii tabia ya watu kuweka makadirio ya bajeti kidogo na kukusanya zaidi au makadirio juu kisha kukusanya chini sana sio nzuri inaonyesha hakuna takwimu sahihi ya vyanzo vya mapato hivyo bajeti zetu ziendane na uhalisia wa tathmini ya vyanzo vya mapato,” alisema Mchengerwa.
Aidha aliongeza kuwa, “katika usimamizi wa rasilimali watu kuna mfumo wa Usimamizi wa Mishahara (HCIMS) na mfumo wa Usimamizi wa Utendaji Kazi katika Utumishi wa Umma (PEPMIS), Mifumo hii imesaidia kurahisisha kazi na uwajibikaji; Mifumo ya Ununuzi wa Umma (NEST) pamoja na ile ukusanyaji wa mapato kama TAUSI, GoTHOMIS na mingineyo itumike ipasavyo katika Halmashauri zetu.”