Nyota wa Ihefu FC, Marouf Tchakei ameanza mazoezi mepesi na timu hiyo baada ya kukosekana kwa takriban majuma matatu kutokana kusumbuliwa na majeraha ya kifundo cha mguu aliyoyapata katika mchezo wa 32 bora Kombe la Shirikisho dhidi va KMC.
Tchakei aliumia Aprili 06, mwaka huu, wakati Ihefu FC ilipoifunga KMC mabao 3-0, Uwanja wa Azam Complex na kumfanya kukosa michezo mitatu mfululizo ambayo ni dhidi ya Simba SC (Aprili 13), Singida Fountain Gate (Aprili 18) na Azam FC (Aprili 21).
Mchezaji huyo mwenye mabao manane ya Ligi Kuu na asisti tatu hadi sasa, amesema ni jambo zuri kwake kurejea mazoezini japokuwa anaendelea na programu za benchi la matabibu.
“Ni vizuri kwangu kurudi na muda sio mrefu naamini naweza kucheza moja kwa moja. Kwa sasa bado sijaanza kujumuika na kikosi cha kwanza na wenzangu kwa sababu nimepewa siku kadhaa hadi pale madaktari watakapojiridhisha niko fiti asilimia 100,” amesema Tchakei raia wa Togo, huku Daktari wa timu hiyo, Shima Shonde amesema hawatafanya haraka nyota huyo kurudi uwanjani kwani majeraha aliyopata yanahitajika uangalifu wa hali ya juu ndio maana wakampa programu binafsi kabla ya kujiunga na wenzake.
Kwa upande wa kocha mkuu wa timu hiyo, Mecky Maxime amesema licha ya umuhimu wa mchezaji huyo katika kikosi, lakini hawatakuwa na haraka ya kumtumia kwa michezo ijayo ili kumpa nafasi ya kupona vizuri na kurejea katika ubora wake.
“Mchezo wetu ujao wa Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Mashujaa tutakaocheza Mei Mosi tutaangalia na fitinesi yake kwa jumla kabla ya kumtumia, ila kama nilivyosema hapo awali sio rahisi kucheza kwa sababu tunahitaji apone vizuri,” amesema Maxime nyota wa zamani wa Mtibwa Sugar na Taifa Stars aliyewahi pia kuzinoa timu za Mtibwa, Kagera Sugar na Cambiaso.
Ihefu FC kwa sasa ipo nafasi ya 11 ikiwa na alama 25 zilizotokana na mechi 24 na mara ya mwisho ilipocheza mchezo wa Ligi Kuu ikiwa ugenini dhidi ya Azam Complex kwa kufungwa bao 1-0 lililowekwa kimiani na Feisal Salum ‘Fei Toto’ lililomfanya nyota huyo wa zamani wa JKU na Young Africans kufikisha mabao 14 msimu huu 2023/24.
Mara baada ya kumaliza na Mashujaa FC katika Kombe la Shirikisho, Ihefu FC itarudi katika Ligi Kuu kwa kuikaribisha Namungo FC mjini Singida siku ya Mei 7.