Boniface Gideon – Tanga.
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo – CHADEMA, Freeman Mbowe amesema panga pangua ya wateule wa Rais hususani Ma DC na Ma RC akisema inachangia kuongeza matumizi Makubwa ya Serikali na kusababisha matumizi mabaya ya fedha na kutaka hatua zaziada zichukuliwe,
Mbowe ameyasema hayo hii leo April 29 mara baada ya kuongoza Maandamano ya Amani kwaajili ya kupinga kupanda kwa gharama za Maisha na kidai katiba Mpya yaliyofanyika katika mitaa mbalimbali ya Barabara za namba jijini Tanga.
Akizungumza na mamia ya Wakazi na wafuasi wa chama hicho, Mbowe pia aliwataka Wananchi kutokuogopa kudai katiba Mpya hukua akisema anakerwa na tabia ya Serikali kuwapa tenda mbalimbali Wakandarasi wa Kimataifa na Makandarasi wa ndani wakibakia hawana kazi.
“Uteuzi na uhamishaji wa viongozi wakuu wa Wilaya na wakuu wa Mikoa inaongeza matumizi Makubwa ya Serikali, CHADEMA tukiingia madarakani tutawaondoa viongozi wote ambao hawajapata ridhaa ya Wananchi,tutahakikisha Viongozi wote wanakuwa wamepata ridhaa ya Wananchi,” alisema Mbowe.
Aidha aliongeza kuwa, “Wananchi msiogope kudai katiba Mpya, Katiba ndio msingi imara wa Uchumi, Siasa ni maisha,Siasa utaikuta kila sehemu, ukienda hospitalini utakuta hali mbaya,vivyo hivyo hata kwenye Sekta za Afya, Elimu na Uchumi utakutana na hali mbaya ,Sera na Sheria zetu zinayumbishwa na kukosa katiba nzuri.”
“Wakandarasi wa Kimataifa hasa kutoka china ndio wanaopewa kazi ya ujenzi wa miundombinu ya Barabara nyingi hapa Nchini kwetu huku wakandarasi wa ndani wakibakia hawana kazi,sisi CHADEMA tukiingia madarakani tutaanza na hilo,” aliongeza Mbowe.
Alisema chama hicho kimejipanga kutengeneza Taifa lenye haki kwenye kila Sekta kwakuweka Katiba Mpya itakuwa msingi imara wa sera mbalimbali
“Viwanda vingi vimekufa,leo hii nguo tunaagiza nje, mpaka mafuta yakula tunaagiza nje,sisi CHADEMA tukiingia madarakani tutaanza na Katiba Mpya,ili tuwe na Taifa lenye haki, tunataka tuwasaidie wakulima ili wafaidike na kilimo Bora,hatutaki viongozi wezi, tunataka kila Sekta mwanchi anufaike na tunà za Taifa hili,” alisema.